KAMATI YAITAKA TANROADS KUZINGATIA VIPENGELE VYA GHARAMA KWENYE MIRADI






 KAMATI YAITAKA TANROADS KUZINGATIA VIPENGELE VYA GHARAMA KWENYE MIRADI


Na Mwandishi Wetu


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha wanaingia mikataba ya ujenzi yenye gharama isiyokuwa na nyongeza za fedha.


Imesema wakandarasi wengi  wanaoingia mikataba ya ujenzi na Tanroads wanakuja na mfumo wa nyongeza za gharama hali inayoisababishia serikali gharama zisizokuwa na tija.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Dart awamu ya pili eneo la Mbagala.


"Serikali imetoa fedha nyingi katika ujenzi wa mradi huu. Jitihada ni nzuri zimefanyika, tumeridhika na kwa sasa kuna maendeleo. Lakini igeni mfumo wa TRC katika ujenzi wa barabara. Wakandarasi wanakuja na mfumo wa nyongeza za gharama hali inayosababisha miradi kuwa na gharama kubwa," alisema Kakoso.


Mbali na kutoa agizo hilo, kamati hiyo iliagiza Tanroads wanapojenga Miundombinu wazingatie uelekeo ya maji kutotiririka kuelekea kwa wananchi.


Pia Tanroads wanapaswa kuimarisha ulinzi katika maeneo ya chini ya madaraja pamoja na mikataba wanayoingia imalizike kwa wakati na kusiwepo na nyongeza ya muda.


Kadhalika, kamati hiyo ilitoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanaitunza miradi ya serikali ili kuleta maendeleo endelevu.


Akizungumza baada ya maagizo hayo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema wameyapokea maagizo hayo na watayafanyia kazi.


Profesa Mbarawa alisema kuhusu mfumo wa nyongeza ya gharama kwa wakandarasi watakwenda kujifunza kwa TRC.


Naye Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatus Mativila akiwasilisha taarifa ya mradi huo alisema ujenzi hadi sasa umefikia asilimia 89.9 na ulipaswa kukamilika Machi 27, mwaka huu lakini mkandarasi ameomba nyongeza ya muda ya miezi saba zaidi   ili akamilishe.


Alisema baada ya kumpokea maombi hayo wanaendelea kuyafanuyia kazi kuhusu uhalaki wake. 

 

"Tathmini iliyofanywa inaonyesha kuwa gharama ya mkataba itaongezeka kutoka Sh. 217.48 bilionii hadi Sh. 253.91 ongezeko hili la asilimia 56.7"alieleza  Mativila.


Alisema sababu nyingine ya kuongezeka kwa bei ya bidhaa mbalimbali zaidi ya makisio ya awali ni maboresho ya usanifu.


"Daraja la Kigogo kuvuka Mto Msimbazi kwenye Barabara ya Kawawa pia halitaweza kujengwa kupitia kandarasi hii kutokana na ufinyu wa bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa haraka awamu ya pili," alisema Mativila.


Alibainisha kuwa ujenzi wa daraja hilo haukuwa sehemu ya kazi zilizokusudiwa kufanywa toka awali.

Mwisho

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao