Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

MATUMIZI ya simu kwa wanafunzi shuleni ambayo yamekuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili kwao, yanaweza kudhibitiwa endapo wamiliki wa shule, walimu na wazazi watasimamia sheria zitakazosaidia kuwabana wanafunzi kumiliki simu.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni wakati wa mahafali ya kwanza kwa darasa la saba na ya saba kwa kidato cha nne katika Shule ya Msingi na Sekondari ya Mwilamvya Wilaya ya Kasulu mkoani hapa na Mkaguzi Mkuu wa Shule Kanda ya Ziwa Magharibi, Adrian Mlelwa.

Mlelwa, alisema kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi hutumia simu katika vitendo viovu na kusahau kutekeleza majukumu ya elimu wawapo shuleni.

Alisema kuwa kwa sasa ni kipindi cha utandawazi, hivyo mawasiliano ni muhimu kwa kila mmoja, japokuwa katika matumizi hayo kuna madhara na faida zake, na wanaoathiriwa na madhara ya matumizi ya simu ni wanafunzi kwa vile wengi wao hutazama picha za ngono na kutumiana ‘meseji’ za mapenzi wakati wa masomo.
“Hatuwezi kuwazuia wanafunzi kutumia simu kuwasiliana na wazazi wao, na hapo ndipo kuna umuhimu wa kuweka sheria kali zitakazowafanya watumie simu vizuri, kuna ulazima kwa wanafunzi kutomiliki simu wanapokuja shule, isipokuwa kuwe na utaratibu wa shule kupata simu moja au mbili ambazo zitakuwa zikitumiwa na wanafunzi kuwasiliana na wazazi wao pindi wanapohitaji,” alisema Mlelwa.

Aidha, Mlelwa alisema kuwa suala la nidhamu ndio chachu ya mafanikio ya wanafunzi, hivyo kuna ulazima kwa walimu na wazazi kufuatilia kwa karibu nidhamu za wanafunzi wawapo ndani na nje ya shule.

“Jifunzeni katika shule za kidini ambazo wanafunzi wake wana nidhamu ya hali ya juu, kitu ambacho huwafanya wawe na matokeo mazuri kitaifa…kama shule ya Kaizilege ya Bukoba, ambayo ni miongoni mwa shule zinazoongoza kitaifa katika ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne,” alisisitiza.

Aidha, aliisifu shule hiyo kwa kufanya vizuri kitaaluma sambamba na kujenga maabara ya kemia, fizikia na baiolojia, jambo linalofanya kutimiza agizo la Rais Jakaya Kikwete la kutaka kila

Sekondari kuwa na maabara.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Sabuda, alisema ili kuwa na kizazi kitakachokuwa na tija kwa taifa, kuna ulazima wa kutatua changamoto zinazokwamisha jitihada za wanafunzi kufikia malengo waliyojiwekea.

“Moja ya changamoto ni migogoro ya wanafunzi na walezi, ambayo chanzo chake ni utandawazi tulionao sasa. Wizara na wazazi watusaidie kupunguza ama kukomesha kabisa matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni,” alisema Sabuda.

Naye Kiongozi wa serikali ya wanafunzi shuleni hapo, Stephano Peter, alisema kuwa simu huleta madhara kwa wanafunzi kwa vile ni chanzo cha kufeli mitihani yao, kwani baadhi hutumia muda wa kujisomea kwa kuongea na simu na wapenzi wao.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji