Membe: Nikiwa Rais Nyerere atafurahi
Lindi/Dar. Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, ametangaza rasmi nia ya kuutaka
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2015 akisema anatosha na kwamba
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere huko aliko atafurahi endapo
atakuwa rais.
Membe aliyasema hayo jana kwenye Viwanja vya Ofisi
ya CCM Mkoa wa Lindi katika hotuba yake ya saa moja kutangaza nia yake
hiyo huku kwa kujiamini kabisa akisema kuwa yeye ndiye Rais wa Tanzania
kwa miaka 10 ijayo.
Alisema katika urais wake, ataboresha elimu,
ataweka msisitizo katika utawala bora, maendeleo ya jamii, uchumi na
masuala mbalimbali ya kisiasa na kidiplomasia.
Huku akishangiliwa na maelfu ya watu waliofika kumsikiliza, alisema amejipima na kuona anaweza.
“Nimetafakari sana, nimeona ninatosha kwa nafasi
hii nyeti…, nafasi adhimu na si ya mzaha japo naona wapo wanaofanya
mzaha. Nimeangalia nikaona hakuna mwingine wa kufanana na mimi.
“Sikukurupuka, zipo nafasi za kukurupuka na wapo wanaokurupuka, lakini si vyema kukurupuka kwa nafasi ya urais,” alisema.
Membe aliyesindikizwa na mkewe Dorcas, alisema
Machi mwaka huu alikwenda Butiama na kuzuru kaburi la Mwalimu na kupiga
goti na kumweleza nia yake ya kuutaka urais.
“Nilipiga goti nikamwambia Mwalimu, navitaka viatu
vyako, alivivaa Mzee Mwinyi (Ali Hassan), Mzee Mkapa (Benjamin) na
Kikwete (Jakaya), sasa nataka kuvaa mimi na nina hakika vinanitosha.
“Ninaamini vitanitosha. Nikamwambia chondechonde,
kama havitanitosha, niambie… timu yangu ya mikoani ikawahi kuniambia
unatosha,” alisema Membe.
Alisema alialikwa na Mzee Mwinyi katika ‘birthday’
yake ya miaka 91 na kati ya mambo aliyomwambia ni kwamba ameongoza
nafasi mbalimbali, lakini hakuwahi kununua uongozi.
Maoni
Chapisha Maoni