Lissu: Marehemu amepiga kura Katiba

MWANASHERIA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amesema mchakato wa kutengeneza katiba mpya ni wa kihistoria kwani jina la marehemu lilipiga kura.
Akifafanua kauli hiyo alisema jina la mjumbe Shida Salum aliyefariki dunia Julai mwaka huu, limo kwenye orodha ya waliopiga kura ya ndiyo wakati kupitisha Katiba inayopendekezwa.

Lissu alisema hayo mwishoni mwa wiki mjini hapa alipotoa mada kwenye mdahalo wa kujadili Katiba iliyopendekezwa inayosubiri kupigiwa kura na wananchi, ambako alihoji ni Katiba Mpya au katiba ya kiimla katika rangi ing’aayo.

“Aliyekuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kundi la 201 kila mmoja anajua kwamba alifariki dunia lakini ukiangalia kwenye orodha ya waliopiga kura (huku akiionyesha kitabu kwa washiriki), anaonekana amepiga kura ya ndiyo.

“…Hii inawezekanaje jamani, ndiyo maana nakubaliana na Rais (Jakaya Kikwete) kuwa hii katiba iliyopendekezwa ni ya kihistoria,” alisema Lissu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA.
Mwanasheria huyo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema kitendo cha baadhi ya wajumbe kupiga kura wakiwa hospitalini ni miongoni mwa matukio yatakayokumbukwa kwa kuweka historia kwani halijawahi kutokea sehemu yoyote ulimwenguni.

Alisema kuwa kuna ushahidi wa barua iliyotoka kwa balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia ikieleza kuwa itakuwa vigumu kwa mahujaji waliohudhuria ibada ya Hija, Makkah kupiga kura lakini cha kushangaza kwenye orodha ya waliopiga kura, mahujaji wamo tena wamepiga kura za ndiyo.
Lissu alisema haijawahi kutokea mteule wa rais kumpinga hadharani kama ilivyotokea kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar (AG), Othman Masoud Othman aliyepiga kura ya hapana baada ya kuona katiba hiyo inapingana na maoni ya wananchi wa Zanzibar hivyo historia itamkumbuka.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CHADEMA, alisema hata kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba na wajumbe wake kususia hafla ya makabidhiano ya katiba inayopendekezwa ni jambo la kihistoria kwa kile alichoeleza kuwa tume hiyo iliyozunguka kwa wananchi na kuandaa rasimu ya kwanza na ya pili hivyo kugomea kwao si jambo la kupuuzwa.

“Haijawahi kutokea Rais wa nchi hii kususiwa na mabalozi wa mataifa makubwa kama Uingereza na Marekani na kila mara tunamsikia anajivunia kufuata misaada huko. Kwenye tukio la makabidhiano ya katiba inayopendekezwa mabalozi hao hawakutokea…

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili tumeshuhudia viongozi wa dini wakisema waziwazi hapana kwa katiba mpya… pia ni mara ya kwanza kwa waziri kuwatukana viongozi wa dini, tulishuhudia Samuel Sitta akiwaita viongozi wetu hawa wa kiroho ni wapuuzi,” alisema Sitta.

Lissu alisema kuwa kuanzia mwanzo wa mchakato wa katiba mpya, kulikuwa na juhudi za mchakato huo kudhibitiwa na serikali ingawa kambi ya upinzani ilipinga juhudi hizo.
Alipotafutwa Katibu wa lililokuwa Bunge Maalum la Katiba Yahya Khamis Hamad kutoa ufafanuzi juu ya hilo, simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani na hata alipotafuwa Katibu Msaidizi, Dk. Thomas Kashilillah, simu yake iliita bila kupokelewa

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao