Profesa Shivji: Migogoro ya ardhi ni adui wa maendeleo ya wananchi
Kwa muda mrefu, Serikali imekuwa ikianzisha mipango, sera, miradi na mikakati mbalimbali yenye lengo kuinua uchumi nchini.
Licha ya mipango hiyo kuwapo, bado kumekuwa na
ugumu katika kufikia mafanikio yaliyotarajiwa kutokana na sababu
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa na mipango na mikakati mingi kwa
wakati mmoja pamoja, hali kadhalika uwapo wa migogoro ya ardhi katika
vijijini vingi nchini.
Wakati kukiwa na ugumu huo, inaelezwa kuwa
asilimia 70 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo, lakini wengi
wanashindwa kufikia malengo kutokana na migogoro ya ardhi.
Baadhi ya mipango ya Serikali ya kuinua uchumi ni
pamoja na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini (Mkukuta),
Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (Mkurabita),
Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDS). Programu ya Kuendeleza
Sekta ya Kilimo (ASDP), Kilimo Kwanza, Uendelezaji Kilimo Ukanda wa
Kusini Tanzania (SAGCOT), Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao
ulianza mwaka 2011-2016 na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Profesa Issa Shivji ni mmoja kati ya waanzilishi
wa taasisi ya utafiti na utetezi wa haki za ardhi inayoitwa HakiArdhi.
Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1994 kwa ajili ya kuhakikisha kuwa
wananchi wanatumia ardhi kwa ajili ya maendeleo kwa kuwa ardhi ni
gurudumu la maendeleo.
Akizungumzia maadhimisho ya miaka 20 tangu
kuanzishwa kwa taasisi hiyo, Profesa Shivji anasema: “Huwezi kuzungumza
mfumo wa umiliki ardhi nje ya mwelekeo na mfumo wa nchi. Jiulize,
unataka nani au kundi gani katika nchi liwe gurudumu la maendeleo.”
Profesa Shivji, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Tume
ya Ardhi iliyoundwa mwaka 1990 ya Rais Ali Hassan Mwinyi kwa ajili ya
kuangalia matatizo na migogoro ya ardhi nchini na baadaye kutoa
mapendekezo.
Tume hiyo ilipendekeza kuwa gurudumu la maendeleo
liwe wazalishaji wadogo, hasa wa vijijini na hivyo lazima wazalishaji
hao washirikishwe katika suala zima la ugawaji wa ardhi.
“Kuna mjadala mkubwa tu na upande mmoja unasema ni
wawekezaji. Sasa kama umeamua wawekezaji ndio watakuwa watu wa
kutuletea maendeleo, lazima upore ardhi kwa wanakijiji na kuwapatia
wawekezaji,” anasema.
“Kama unakubali kwamba mchango wa wawekezaji
hautakuwa mstari wa mbele na wazalishaji wadogo ndiyo watapewa
kipaumbele, lazima uondoe hofu juu ya ardhi kwa wazalishaji hao.”
Anasema msingi mkuu wa kuanzisha Taasisi ya
HakiArdhi mwaka 1994 ni baada ya kuona mapendekezo makuu ya tume hiyo
kutozingatiwa na Serikali.
“Inatakiwa iwe hivi. Serikali ikitaka ardhi kwa
manufaa ya wananchi, lazima iwashirikishe wananchi husika na waelezwe na
kukubali,” anasema.
Maoni
Chapisha Maoni