Ulaya wasikitishwa mchakato Katiba

UMOJA wa Ulaya (EU), umesikitishwa na Tanzania kutoitumia fursa ya uundwaji wa Katiba mpya kuiondoa adhabu ya kifo.
EU, imeeleza hayo jana katika taarifa yake kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku ya kupinga adhabu ya kifo na kueleza kuwa, itaendelea kupaza sauti hadi adhabu hiyo itakapofutwa.
Pia, EU imeeleza kuwa Tanzania bado ina nafasi ya kuiondoa adhabu hiyo katika katiba pindi itakapopigiwa kura.
EU na Baraza la Ulaya, limeeleza kuwa baada ya kutiliana saini na kuunganisha nguvu, watahakikisha wanaendelea kupinga adhabu hiyo katika kesi zote ili dunia iikomeshe na kulinda ulinzi wa haki za binadamu.
Umoja huo umeeleza kuwa jumuiya hiyo italinda na kuhakikisha hakuna mwanachama anayetumia adhabu hiyo na kuleza kuwa mwaka huu idadi ya watu waliohukumiwa adhabu hiyo imeongezeka.
Aidha, EU imetoa wito kwa kwa nchi za Afrika kuendelea kukubali itifaki na mikataba ya kutetea haki za binadamu na kukomeshwa adhabu.
Pia, EU iliyapongeza mashirika mbalimbali ya kiraia yanayofanyakazi ya kutaka kupingwa kwa adhabu hiyo na kuyataka yaendeleze juhudi za kuhamasisha.
Walieleza kuwa tangu Tanzania ipate uhuru imekuwa ikitiliana mikataba inayohusu kutetea haki za binadamu ndani ya mfumo wa Umoja wa Afrika na pia ni mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), na Mkataba wa Kimataifa wa Uchumi, Jamii, na Haki za Kitamaduni (ICESCR).
Adhabu ya kifo hapa nchini mara ya mwisho ilitekelezwa mwaka 1995, na kwa upande wa nchi nyingine adhabu hiyo imekuwa ikiendelea kutolewa huku taarifa zikitaja idadi ya vifo kufikia 778 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15, ambako Iran na Iraq zinaongoza.
Nacho Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimetaka kurekekebishwa kwa ibara ya 33 katika katiba pendekezwa inayoruhusu kuendelea kwa adhabu ya kifo.
Wito huo ulitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa kituo hicho, Imelda Lulu Urio, wakati alipokuwa akitoa tamko lao kuhusu maadhimisho ya siku ya kupinga adhabu ya kifo duniani inayofanyika kila mwaka ifikapo Oktoba 10.
Urio, alisema wanasikitishwa kuona kuwa licha ya kuwepo kwa kampeni ya kufuta adhabu hiyo, bado imeendelea kuwepo katika katiba iliyopendekezwa ambayo imepitishwa na Bunge Maalum la Katiba hivi karibuni.
“Ibara ya 33 inasema kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii, hifadhi ya maisha yake kutoka katika serikali na jamii kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Pia katika Ibara ya 95(1)(c)imempa Rais mamlaka ya kubadilisha adhabu ya kifo kuwa adhabu ya kifungo cha maisha.
Kwa maana hiyo, bado katiba hii pendekezwa inaendeleza uwepo wa adhabu ya kifo kikatiba, ambayo ni kinyume na haki za binadamu hususani katika karne hii ambayo nchi nyingi zimefuta adhabu.
Hata hivyo alisema katika kuadhimisha siku hiyo, Kituo kinashauri Ibara ya 33 ya katiba pendekezwa kufuta na kuondoa kabisa neno kwa mujibu wa sheria za nchi ili kuhakikisha kuwa haki ya kuishi inakuwepo bila pingamizi au kuminywa na sheria yoyote.
Pia Mkurugenzi huyo alitaka Tanzania kujifunza kwa nchi nyingine duniani ambazo hazitekelezi adhabu ya kifo ni kwa jinsi gani zimekuwa zikishughulikia watu wenye makosa ya kuua

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao