Ukawa waanza kugawana Majimbo
Moshi. Baada ya kumalizika kwa Bunge la Katiba, hasira za Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) dhidi ya CCM zimehamia kwenye Uchaguzi
Mkuu wa 2015, safari hii ukiunda kamati maalumu kutafuta namna ya
kumsimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana majimbo.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia ametoa
maelezo hayo alipokuwa akizugumza na gazeti hili katika mahojiano
maalumu hivi karibuni.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,
alisema tayari kamati zimeundwa na zinaendelea na kazi ya kuratibu
mpango huo mahususi, unaolenga kuiondoa CCM madarakani.
“Lengo letu ni kuhakikisha Ukawa ina nguvu ya
kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na katika mpango huo, vyama
vitaachiana majimbo na viti vya udiwani kulingana na nguvu ya chama
katika sehemu husika,” alisema.
Ukawa; umoja ulioanzishwa Februari mwaka huu ukiwa
ni kikundi shinikizi katika mchakato wa Katiba katika siku za mwanzo za
Bunge Maalumu la Katiba, unaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema,
CUF na NLD.
Mbatia alisema anaamini kwa mkakati huo uliopangwa na Ukawa, CCM itakuwa na wakati mgumu katika uchaguzi mkuu ujao.
“Sasa hivi ziko kamati zinaaendelea na maandalizi
ya namna ya kushirikiana katika uchaguzi mkuu ujao na nataka
nikuhakikishie siku za Serikali ya CCM zinahesabika,” alisema Mbatia na
kuongeza:
“Kamati hii inatafiti ni namna gani bora ya
kuachiana madiwani, wabunge na rais ili tusimamishe mgombea mmoja katika
kila eneo na tutakubaliana nani asimame wapi.”
Mbatia alisema uchaguzi mkuu ujao utamalizika kwa
wabunge wengi wa upinzani kuingia bungeni na iwapo mambo yatakwenda kama
walivyopanga, CCM kinaweza kuwa chama cha upinzani.
“Kwa sasa wagombea kutoka Chadema, NCCR-Mageuzi,
CUF na NLD ni ruksa kutangaza nia, lakini kamati yetu itasema nani
miongoni mwao ateuliwe kupeperusha bendera ya Ukawa,” alisema.
Mbatia aliwahakikishia Watanzania kuwa ushirikiano
wa vyama hivyo si nguvu ya soda na kusisitiza kuwa wanaofikiri
ushirikiano huo utavunjika kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015 ni ndoto za
mchana.
“Kwanza tumekwishaunda Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, tuko pamoja na lengo letu tunakuwa na ushirikiano ambao
umeonekana tangu Bunge la Jamhuri, Bunge la Katiba na sasa hivi Ukawa.”
Maoni
Chapisha Maoni