Mkapa aongoza mazishi ya Meja Jenerali Lupogo

Rais mstaafu akiweka shada la mauwa kwenye kaburi la meja Gerali msitafu Herman Lupojo wakati wa Mazishi
RAIS mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa jana aliwaongoza viongozi mbalimbali na mamia ya waombolezaji katika mazishi ya Meja Jenerali mstaafu Herman Lupogo kwenye makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange pamoja na Jenerali Mstaafu Robert Mboma.
Akisoma risala mara baada ya mazishi, Mwakilishi wa JWTZ, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, alisema marehemu alifariki dunia Oktoba 19 mwaka huu kwa ugonjwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo alikokuwa akipata matibabu.
Alisema, marehemu alimaliza elimu ya Kidato cha sita katika shule ya Sekondari Pugu mwaka 1956, baadaye akapata Stashahada ya Ualimu na Shahada ya kwanza ya Sanaa katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.
“Marehemu alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania mnamo Julai 23, 1965 na kutunukiwa Kamisheni Januari 21, 1966 na baadae kwa nyakati tofauti alipandishwa vyeo hadi kufikia cheo cha Meja Jenerali Februari 9, 1983 ambacho alistaafu nacho jeshini,” alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya marehemu kustaafu aliendelea na shughuli mbalimbali za kujenga taifa ikiwamo kuwa Mkuu wa Mkoa Iringa mwaka 1990, Mwenyekiti Chuo cha Diplomasia 1987 hadi 1991, Mkurugenzi Mtendaji wa AICC 1993.
“Pia alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania(TACAIDS), 2001 hadi 2014, marehemu mara kwa mara alienda kushiriki kutoa mihadhara kama mwalimu wa kualikwa katika vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya Jeshi ikiwamo Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC),” alisema.
Aidha, alimalizia kwa kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Maofisa, Askari na Watumishi wa Umma wa JWTZ, kutokana na msiba mzito uliotokea na kwamba sio pigo kwa familia yake, bali kwa ndugu, jamaa, majirani, jeshi na Taifa kwa ujumla.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao