"UJENZI WA MELI MPYA NA CHELEZO KIGOMA KUFUNGUA SOKO LA BIASHARA KIMATAIFA" WAZIRI MBARAWA
"UJENZI WA MELI MPYA NA CHELEZO KIGOMA KUFUNGUA SOKO LA BIASHARA KIMATAIFA" WAZIRI MBARAWA
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame
Mbarawa, amesema uwekezaji wa kampuni ya kizawa ya Dar es Salaam Merchant Group
katika ujenzi wa chelezo na meli mpya mkoani Kigoma utaongeza uwezo wa Tanzania
kujenga na kukarabati meli nchini, huku ukifungua fursa za biashara na huduma
za ujenzi wa meli kwa nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika, ikiwemo DRC na Zambia
Prof. Mbarawa ameyasema hayo baada ya
kukagua eneo la Bulombora Mkoani Kigoma linalojengwa chelezo cha kampuni hiyo,
akisema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi
kushiriki katika uwekezaji wa miundombinu na huduma za usafiri wa njia ya maji
hatua ambayo itaongeza uwezo wa wazawa katika ujenzi na ukarabati wa vyombo
vinavyosafiri kwa njia ya maji
Amesema kampuni hiyo, iliyoshiriki
katika ujenzi na ukarabati wa meli ikiwemo MV Liemba, imeanza maandalizi ya
ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo,
Meli ambayo itaongeza uwezo wa usafirishaji katika Ziwa Tanganyika na kuchochea
biashara kati ya Kigoma, Katavi, Rukwa
na nchi jirani
Prof. Mbarawa amesema mradi huo
unaendana na azma ya Serikali ya kuwawezesha wazawa kushiriki katika miradi
mikubwa ya maendeleo na kuongeza uwezo wa ndani katika sekta ya uchukuzi,
akiahidi Serikali kuendelea kutoa ushirikiano ili mradi ukamilike kwa wakati na
kwa viwango vinavyotakiwa
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa
Dar es Salaam Merchant Group, Bw. Rayton Kwembe, amesema sehemu ya kwanza ya
chelezo inatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, huku maandalizi ya ujenzi wa meli
mpya yakiendelea
Eneo hilo, lililopo kilomita 25 kutoka
Kigoma mjini, lina ukubwa wa mita za mraba 95,000 na litakuwa na maeneo ya
kutengeneza na kuunganisha vitalu vya meli, kujengea meli pamoja na floating
dock kwa ajili ya kuingiza na kushusha meli kwenye maji
Aidha, kampuni hiyo imesema imeanza
kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini katika ujenzi wa meli, ikiwemo viti,
makabati, vitanda na samani nyingine. Hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya
bidhaa za ndani, kukuza ujuzi wa wazawa na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka
nje






Maoni
Chapisha Maoni