Pinda akerwa na ushirikina, dawa za kulevya

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa dini nchini kuitumia mikutano ya mahubiri kutoa elimu kwa waumini wao na wananchi kwa ujumla kuachana na imani za kishirikina za kukata viungo na  kuwaua walemavu wa ngozi (albino ).
Pia, amewaomba kutumia mahubiri hayo kutoa elimu juu ya athari za dawa za kulevya kwa waumini wao na Watanzania wote kwa ujumla.
Pinda alitoa wito huo jana wakati wa ibada ya uzinduzi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Mashariki uliyofanyika kwenye makao makuu ya jimbo hilo, Mbagala Chamazi. Jimbo hilo linajumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Lindi, Mtwara na Pwani.
Akizungumza mbele ya viongozi hao wa dini kutoka ndani na nje ya nchi, Pinda alisema Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya matumizi ya dawa za kulevya hasa kwa vijana.
“Nchi yetu imekuwa ikitajwa kwamba inatumika kwa kasi katika kusafirisha dawa za kulevya. Ni jana tu tumesikia taarifa katika vyombo vya habari zikitaja kwamba meli moja ya Tanzania imekamatwa huko Uingereza ikiwa imebeba tani tatu za dawa za kulevya,” alisema na kuongeza: “Niwaombe sasa viongozi wa taasisi zote za dini, tuungane na Serikali kutoa elimu juu ya athari za biashara ya dawa za kulevya na matumizi yake katika jamii. Ninawasihi tuhakikishe kwenye mikutano yote tunayoifanya tusimalize bila kutoa elimu kuhusu athari za dawa za kulevya kwa waumini wetu na umma kwa ujumla.”
Pinda alisema, viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuwalea zaidi vijana ili wasijiingize kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu wao ndiyo kundi kubwa zaidi miongoni mwa waumini.
Akizungumzia mauaji ya albino, aliwaomba viongozi wa dini kushirikiana na Serikali kukemea kwa nguvu zote vitendo hivyo.
“Tangu mwaka 2006 kumetokea mauaji ya watu 46 niwaombe tena taasisi zote za dini zitusaidie kuondoa au kubadili imani hizi za kishirikina miongoni mwa jamii. Ninaamini tukiunganisha nguvu zetu kwa pamoja dhidi ya fedheha hii tutashinda,” alisisitiza.
Askofu Kiongozi wa kanisa hilo, Dk Issack Nikodemo aliwataka waumini wa Kikristo kuomba kwa ajili ya amani ya Taifa hasa katika kipindi hiki ambacho linajiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.
Mwenyekiti wa Jimbo la Kigoma, Charles Katare alisema kanisa hilo lipo tayari kumchangia Waziri Mkuu fedha za kununua fomu kugombea urais, kwani wamesikia anataka kuwania nafasi hiyo.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao