Ukawa wasumbua vichwa vya Baadhi ya Wabunge Dodoma

KATIKA hali inayoonekana kama kutaabishwa na wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba Swmweli Sita
Samuel Sitta, jana aliamua kueleza hali halisi ilivyo kwa takribani dakika sita akiwa ndani ya ukumbi wa Bunge wakati mjadala wa katiba ukiendelea  na kuwaita  wajumbe kuwa  ni waigizaji.
Hatua hiyo ya Sitta, ilibadili upepo wa Bunge kwa muda, kwani baadhi ya wachangiaji wa mjadala wa sura za rasimu ya katiba, nao waliamua kuanza kujadili hoja na kujikita kuwataka wana  UKAWA kuwa wakeli.
Miongoni mwa wajumbe waliochepuka kwenye mjadala na kuwajadili UKAWA ni Mwenyekiti wa UPDP, Fahami Dovutwa, ambaye alizungumzia kuhusu makubaliano ya kikao baina ya vyama vinavyounda Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD), na Rais Jakaya Kikwete.
Licha ya kuwafurahisha wajumbe wa CCM, Dovutwa alijikuta akitofautiana na Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo (UDP), pale alipokiri kwamba yeye, Cheyo na Augustine Mrema (TLP), hawakusaini baadhi ya vipengele vya
makubaliano kama ilivyodaiwa na viongozi wa UKAWA.
Dovutwa, alitaja sababu ya kutosaini baadhi ya vipengele hivyo kuwa ni kutokana na masharti ya mtego ya ghafla ya UKAWA kutaka Bunge hilo lisitishwe, jambo ambalo ni kinyume na tangazo la Serikali Na 254, lililowekwa kwa mujibu wa sheria.
Vituko hivyo, vilianza kwa Sitta kuwashambulia baadhi ya wasomi wanaokosoa uendeshaji wake wa Bunge, akisema ni watu wanaohusiana na UKAWA, ambao kazi yao kubwa ni kuzuia kabisa katiba mpya isipatikane.
Bila kumtaja kwa jina mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE), Prof. Kitila Mkumbo, aliyemnukuu jana asubuhi akimkosoa kupitia kituo cha runinga cha Star, Sitta alisema;
“Kuna watu wanajiita wasomi nadhani wanahusiana na hao wanaojiita UKAWA, ambao jitihada yao kubwa sana ni kuzuia kabisa katiba isipatikane.
“Leo nimemsikia mmoja anasema kwamba, kupiga kura itakuwa Sitta anavunja sheria ya uchaguzi. Sisi hatupigi kura ya uchaguzi, tunapiga kura ya uamuzi kuhusu suala ambalo wajumbe hao wana haki ya kupiga kura na kushiriki katika kuamua juu ya katiba,” alisema.
Sitta aliongeza kuwa, ndio maana hata katika kamati walipigisha kura kwa wajumbe waliokuwa hospitalini, kwamba hilo ni jambo tofauti kabisa wala wajumbe hawapaswi kufadhaika kwa sababu ni kawaida ya watu,
wameamua kujisemea wanavyotaka.
Mwenyekiti huyo, hakuishia hapo kwani baada ya dakika chache alisimama tena na kusema; Waheshimiwa wajumbe nadhani mtakuwa mmesikia kupitia vyombo vya habari kwamba, UKAWA wanataka kunishtaki katika Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai iliyoko The Hague, Uholanzi.
“Sasa sijui kama wenzangu mnakiona kitu kimoja ambacho mimi nakiona, baadhi ya viongozi wa UKAWA wana kipaji cha dhahiri cha uigizaji kabisa. Ni waigizaji wazuri,” alisema na kuongeza;
Ebu fikirieni vituko vyao…tulipokuwa hapa mwanzoni, tumevutana siku 18 kuhusu kura ya wazi au siri-siku ya kuzikubali kanuni, watu hawa waliopigania kufa na kupona kupiga kura ya siri, wakapiga kura ya wazi.
“Wakaleta tishio kwa kumtuma mwenzao mmoja akaleta hoja binafsi kwamba Bunge hili lisiendelee hadi hati ya Muungano ipatikane…tukaleta nakala, wakasema hapana mmeghushi saini ya hayati Karume.
“Ilipokuja halisi kutoka mahala pa usalama tarehe 16 Aprili, wakasusia Bunge hadi leo. Juzi mheshimiwa Rais alivyo muungwana, alikutana nao mara mbili zaidi ya saa saba, walifikia maafikiano, wakatoka hapo siku moja baadaye wamekana yale yaliyotokea hapa Dodoma mbele ya Rais,” alisema.
Sitta aliwataka wananchi waendelee kuwapima watu hawa, kwamba yeye anashindwa kuwaelewa kabisa.
“Najua kule Marekani walipata kutokea viongozi ambao ni wacheza sinema kama Ronald Regan…kama Schwarzenegger alikuwa gavana wa California, lakini ile ni nchi tajiri wanaweza kuhimili viongozi ambao wanafanya mzaha mzaha, sisi ni nchi masikini, hatuwezi kuhimili.
“Wananchi wajue hivyo. Kwa hiyo mimi natoa ushauri kwamba mwakani watakaposhindwa vibaya uchaguzi kwa tabia zao hizo basi warejee fani ambayo Mwenyezi Mungu amewajalia, nayo ni uigizaji,” alisema Sitta.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji