TANZANIA YASHAURIWA KUWEKEZA KATIKA MAENDELEO YA WATU WAKE


TANZANIA inatakiwa kuwekeza zaidi katika watu wake ili kuweza kufikia maendeleo ya kweli na endelevu.

Imesemekana, kuwekeza katika watu kumethibitisha kuwa moja ya sababu kubwa ya kufikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya mataifa mbalimbali na pia kuwa kati ya mambo muhimu yanayozingatiwa na wawekezaji wanapochagua maeneo ya kuwekeza.

Kauli hiyo ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF), Dkt. Hoseana Lunogelo, alipokuwa akiongea wakati wa mkutano watatu wa kitaifa wa taasisi hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

"Kwa kuwekeza katika watu, Serikali itahakikisha kuwa wananchi wanawezeshwa kuendesha maisha na kuwa wenye mchango kwa jamii," alisema Dkt.Lunogelo. Alisema kuwa kuwepo kwa nguvukazi kubwa yenye ujuzi ni faida kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Alisema kuwezeshwa huko kunaleta ujuzi, maarifa na ufanisi ambao huimarisha ubora wa nguvukazi. "Nguvukazi yenye ujuzi ni muhimu sana katika kuhakikisha kuwa rasilimali zinatumika kwa ufanisi, watu wanapata mahitaji yao ya msingi na pia kukua kwa uchumi," alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kwa changamoto za maendeleo zinazoikabili Tanzania kwa sasa, ni muhimu kuendeleza watu wake ili kuweza kupambana na changamoto hizo. Alisema elimu pamoja na afya ya watu kama vitu muhimu vinavyojenga uwezo na nguvu ya kitaifa kuendeleza uzalishaji na ushindani wa nchi.

Wakiwasilisha mada kuhusu kuporomoka kwa kiwango cha elimu na suluhisho lake katika mkutano huo, Profesa Suleman Sumra na Dkt. Joviter Katabaro, walisema ni muhimu kwa Serikali kufahamu kuwa kuna matatizo na kwamba ni lazima kuzingatia ubora wa elimu katika mipango na utekelezaji.

"Inawezekana kutoa elimu bora katika shule zetu," walisema na kuongeza kuwa hakuna njia ya mkato isipokuwa kutumia maamuzi yanayotokana na tathmini na tafiti za kina.

Walisema katika hoja yao kuwa ni muhimu kwa nchi kuzingatia na kutoa kipaumbele kwa walimu.

"Elimu bora inaweza kupatikana kama tutakuwa na idadi inayotakiwa ya walimu, waliotayarishwa vyema na wenye motisha," walisema.

Kongamano hilo lililofunguliwa na Rais Jakaya Kikwete, lilihudhuriwa na wasomi wa ndani na nje ya Tanzania, maofisa wa serikali, wadau wa maendeleo, wabunge, mashirika ya kijamii na sekta binafsi.Tangu kuanzishwa kwake miaka 20 iliyopita, ESRF imekuwa ikijihusisha na masuala ya sera za kijamii na uchumi pamoja na kutoa  ushauri kwa serikali.

Ikifanyakazi na wadau wengine, taasisi hiyo imeweza kushiriki katika kutengeneza na kutathmini mipango mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya ESRF, Philemon Luhanjo, alisema taasisi hiyo imefanyakazi kubwa ya kujenga uwezo wa utafiti na uchambuzi wa sera mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.

"Changamoto kubwa tuliyonayo si tu ya maendeleo bali ya mabadiliko‚ lazima tuhakikishe kuwa kukua kwa nchi yetu kunaendana na ustawi wa watu," alisema.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao