SERIKALI KUVIHAKIKI VYAMA VYA KIJAMII
SERIKALI imedhamiria kuanza mchakato wa kuhakiki vyama vya kijamii ili kuboresha huduma zinazotolewa na vyama hivyo nchini tangu kuanzishwa kwake.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Isack Nantanga, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema uhakiki huo utaanza rasmi Oktoba mwaka huu ambapo vyama visivyo na sifa ya kuendelea kuwa katika Daftari la Msajili vya Vyama vya Kijamii, vitafutwa kabisa.
Akizungumzia sababu zinazoweza kusababisha vyama hivyo kufutwa katika daftari hilo, alisema ni pamoja na kutolipa ada za mwaka kwa wakati na kutowasilisha kwa Msajili taarifa za kila mwaka za utendaji kazi wa chama.
Sababu nyingine ni chama kufanya shughuli tofauti na zile ambazo ziliandikishwa kwenye katiba ya chama husika.
"Ili kuvishirikisha vyama husika, kabla ya kuanza uhakiki huu Wizara itachapisha katika baadhi ya magazeti majina ya vyama vyote vya kijamii vilivyopo katika kumbukumbu za daftari hilo.
"Baada ya kutangaza majina hayo, kila chama cha kijamii kitatakiwa kuhakikisha kinatekeleza matakwa ya kisheria ya kulipa ada ya mwaka na kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Kijamii taarifa inayohusiana na mapato, matumizi ya fedha ya chama kama Sheria inavyotaka," alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya kipindi cha miezi mitatu tangu kutangazwa tangazo hilo, Wizara itaanza kuchukua hatua za kisheria ikiwemo ya kukifuta chama husika ambacho kitashindwa kutekeleza maelekezo hayo katika daftari hilo.
Alisema pamoja na taarifa ambazo zitapatikana katika uhakiki huo, zitawezesha kuanzishwa kwa Kanzi Data ya kisasa ya vyama vya kijamii ambayo itasaidia kuboresha mawasiliano kati yao na Msajili wa Vyama na vyama hivyo.
"Hadi sasa, daftari hilo linaonesha kuna vyama vya kijamii 9,554 kote nchini, kati ya hivyo vya kidini 956 na vingine 8,598...Wizara hii ndiyo yenye jukumu la kusajili na kusimamia uendeshaji wa vyama hivyo nchini kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Kijamii Sura 337, iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002," alisema.
Vyama vinavyosajiliwa chini ya Sheria hiyo ni pamoja na vya kidini, kitaaluma, vyama vya starehe na burudani.
Maoni
Chapisha Maoni