Katiba ni mali ya wananchi, waielewe
Tunaendelea na mfululizo wa makala haya kuhusu Katiba Inayopendekezwa baada ya kumaliza sehemu ya pili wiki iliyopita.
Ni muhimu kuendelea kusisitiza kuwa siyo sahihi kupigia kura ya “Ndiyo”au “Hapana” Katiba Inayopendekezwa wakati bado haifahamiki kwa wananchi, haijawafikia wananchi na bado muda wa kuelimisha kwa umma ni mfupi kumwezesha kila mtu kuisoma, kuichambua, kuielewa na kuitumia.
Tunaendelea kusisitiza tena kuwa kila mtu ana haki na anastahili kuijua, kuisoma ama kuelimishwa na kuwa na nakala yake ili kwa wakati wake ajisomee binafsi kwa uelewa zaidi. Tunaendelea kusisitiza tena kuwa idadi ya nakala zilizotolewa hazikidhi haja ya kuwahabarisha, raia walio wengi kuijua, kuielewa na kuitumia Katiba hii kwa minajili ya kuipigia kura.
Tunaomba na kuitaka mamlaka husika kutuchukulia sote kuwa tuna haki na wajibu wa kuijua, kuielewa, kuichambua na kisha kuipa uhalali ama kuikataa kwa hoja za uhakika.
Mjadala wa wiki hii katika kipindi cha Malumbano ya Hoja kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV uligusa pamoja na mambo mengine hoja ya mama mmoja aliyedai kuwa kina mama wa vijijini wana kazi nyingi hawatapata muda wa kusoma Katiba, kwa hiyo wakikusanywa katika vikundi wakasomewa, inatosha! Ilionekana kama mama aliyetoa kauli hii ni mtumishi wa Serikali na kwa kauli hii imethibitisha kuwa Serikali haina nia ya dhati ya kutaka ushiriki wa wananchi katika mchakato wa Katiba. Awali, tumeambiwa tutoe maoni yetu kwenye tume ili yatumike kuandika Rasimu ya Katiba.
Uandishi unaonekana kuacha zaidi ya mambo 20 kama yalivyoainishwa na Jukwaa la Katiba, wanaharakati na hata na baadhi ya taasisi za kidini.
Katika mazingira yasiyolingana wala kupangwa, wiki hii kumekuwa na matukio yaliyoletea wanavijiji na vitongoji vya Kata ya Unyamikumbi katika Manispaa ya Singida Mjini kupata fursa ya kutoa kero zao katika masuala mbalimbali ya maendeleo na suala la katiba lilijitokeza pia.
Katika hali ya urahisi kabisa wananchi hawa, wake kwa waume na wengi wakiwa wazee waliuliza kama wana haki ya kuwa na katiba. Waliuliza pia kama wana haki ya kuijua katiba katika lugha yao ili wabaini kama kweli inawahusu ama la.
Wananchi pia wanataka kujua kama huduma mbalimbali zinazotolewa na serikali ni haki zao ama ni huruma tu ya Serikali kwao.
Maswali ya aina hii yanaashiria kuwa watu hawa wanahitaji kujua maana ya katiba na wanataka kujua kama kero zao zimo ndani ya misingi ya kikatiba ama la na kama ndivyo wafanye nini kupata majibu sahihi kwa maswali yao.
Wakati wa kufikiri kuwa wananchi wanaoishi vijijini ni wajinga na hawana haki ya kujua hata yale wanayostahili, umepita! Maswali yao yanaashiria kuwa wana haja na kuelewa Katiba na ya kuwa kipindi hiki hakitapita bila kufikiwa na elimu hii.
Maoni
Chapisha Maoni