USHAWISHI: Lowassa amponza profesa wa Udom
Dar es Salaam. Profesa wa Chuo Kikuu cha Dodoma
(Udom), Peter Kopoka amebanwa na uongozi wa chuo hicho kutokana na
kushiriki maandamano ya kwenda nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa kumshawishi achukue fomu ya kugombea urais.
Profesa huyo akiwa na wahadhiri pamoja na watu wengine walioelezwa kuwa ni wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Dodoma walifanya maandamano hayo Machi 22, mwaka huu.
Kutokana na tukio hilo, uongozi wa Udom umemtaka
ajieleze kwa nini ameshiriki harakati hizo za kisiasa huku akijua kuwa
ni mtumishi wa umma anayepaswa kuwahudumia watu wenye itikadi tofauti.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula alisema kwa kuwa jambo hilo lilionekana kukiwakilisha chuo katika masuala ya siasa, uongozi ulilazimika kumhoji mhadhiri huyo.
“Ametuandikia barua ya kujieleza na kubainisha kuwa alikwenda yeye binafsi na siyo kama mwakilishi wa chuo. Lakini mambo haya ni magumu sana kutofautisha. Mimi kwa mfano, siwezi kwenda sehemu halafu nikasema sikwenda kama mkuu wa chuo kwa sababu siwezi kutofautisha hilo. Lakini tumechukua maelezo yake na tumeyahifadhi,” alisema Profesa Kikula.
“Maandamano hayo yalifanyika mtaani. Huko walikuwa wanavunja sheria za nchi, kama hayakufuata sheria, Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka ya kudhibiti au kuruhusu jambo kama hilo kufanyika,” alisema. Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Profesa Kopoka alikiri kuandika barua hiyo na kueleza kuwa alichokifanya ni kutekeleza haki yake ya uraia ya ushiriki katika utawala wa haki na demokrasia nchini.
“Nimefanya hivyo. Nilikwenda kutokana na imani yangu kutokana na vile ninavyomfahamu Lowassa. Sikuwa peke yangu. Ni kama ilivyoripotiwa, walikuwapo pia wahadhiri kutoka vyuo vikuu vya Mtakatifu Yohana (St. John) na Mipango,” alisema Profesa Kopoka.
Alisema pamoja na kufanya hivyo, suala hilo halijaathiri utendaji wake wala mkataba wake wa ajira.
Mfululizo wa kukanusha
Siku nne baada ya maandamano hayo, viongozi wa Serikali za wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali walijitokeza na kukanusha habari hiyo kwa maelezo kuwa waliofanya hivyo hawakuwa wanafunzi na wala suala hilo halikupata baraka kutoka vyuoni.
Katika taarifa ya pamoja ya marais wa serikali za
vyuo vikuu hivyo vilivyomo mkoani humo iliyosomwa na Rais wa St. John,
Daniel Daniel imepinga kushiriki kwao na kubainisha kuwa waliofanya
hivyo ni watu wa mtaani.
Maoni
Chapisha Maoni