Wafunga barabara kudai misaada Kahama

Kahama. Waathirika wa mvua ya mawe ya barafu iliyosababisha vifo vya watu 46 katika Kijiji cha Mwakata wilayani Kahama jana alfajiri walifunga barabara kuu ya Kahama-Dar es Salaam- Mwanza na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Wakazi hao walifikia hatua hiyo wakitaka kuishinikiza Serikali kuwapa msaada wa mahema ya kujihifadhia baada ya nyumba zao kubomolewa na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali ambayo ilijeruhi zaidi ya watu 90 wiki iliyopita.
Kufungwa kwa barabara hiyo kulitokana na kuwapo kwa dalili za kunyesha mvua kwenye eneo hilo ambalo sehemu yake kubwa haina nyumba kwa sasa kutokana na tufani hiyo.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Selemani Kulwa alisema jana asubuhi kuwa tatizo la wananchi wa eneo hilo ni ukosefu wa makazi, hivyo baada ya kufika shuleni walishangaa kuona shehena ya misaada imefungiwa kwenye vyumba vya madarasa, yakiwamo mahema .
Kutokana na hali hiyo, wananchi hao waliamua kufunga barabara kwa mawe na magogo kushinikiza Serikali itoe mahema hayo ili wananchi wayatumie kujihifadhi kwa kipindi hiki cha mvua, baada ya nyumba zao kubomoka.
Hata hivyo, askari wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kahama, Leonard Nyandaho walifanikiwa kutuliza ghasia hiyo kwa kuyaondoa magogo hayo, huku wakiwataka wananchi hao kwa kuwa hakuna uhusiano na utoaji wa misaada na malalamiko yao wanapaswa kuyapeleka kwa viongozi wao.
Baada ya kauli hiyo ya polisi, wananchi walitulia na alipowasili Mbunge wao wa jimbo hilo la Msalala, Ezekiel Maige walitoa ushirikiano kwa kushiriki kufungua barabara.
Kwa upande wake, Maige alisema tatizo lililopo eneo hilo ni mahali pa kuishi hasa inaponyesha mvua na ndiyo sababu ya watu hao walipandwa na jazba baada ya kufika shuleni na kushindwa kuelewa sababu za maturubai kuwapo hapo bila ya wao kupewa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu, Isabela Chilumba ambaye ni mmoja wa timu inayomsaidia mkuu wa wilaya kuratibu shughuli zote za utoaji wa misaada katika eneo hilo, alisema kuwa walikubaliana misaada yote ya mahema itolewe kuanzia jana asubuhi, lakini alishangazwa na wananchi hao kugeuka na kutaka wapewe tena.
“Kimsingi tulikubaliana nao kwamba kesho asubuhi (leo) tuwape mablanketi na mahema kwa kuwa tayari tulikuwa tumepokea kiasi ambacho kingetosha angalau wachache kulingana na idadi ya waathirika tuliyonayo… sasa ninashangaa hawa wananchi kubadilika wakishinikiza wapewe usiku na kufunga barabara,” alisema Chilumba.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya aliwataka wananchi wawe watulivu kwa kuwa ugawaji wa misaada unafuata taratibu siyo kutoa ovyo kwa kuwa hata wasiolengwa wanaweza kutumia nafasi hiyo kupata. Alisema utaratibu wa utoaji misaada hiyo umeingiliwa na wanasiasa, hali ambayo inakwamisha utendaji wa serikali kuwasaidia waathirika hao.
Pamoja na hayo, misaada iliyopo ni mingi ikiwamo vyakula vilivyotolewa na watu mbalimbali, taasisi za watu binafsi na za umma.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji