Watoto 18 waliofungiwa Moshi wadai kubebeshwa matofali mgongoni
Moshi. Jeshi la Polisi wilayani hapa, limedai kuwa watoto waliokutwa ndani ya nyumba katika eneo la Pasua, Manispaa ya Moshi siyo wakazi wa Kilimanjaro na walikuwa wakiishi kwenye mateso makubwa.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela imeeleza kuwa hayo yalibainika katika mahojiano baina ya watoto na askari wa dawati la jinsia.
Alisema watoto hao wanatoka mikoa mbalimbali ikiwamo Tanga, Mara, Kagera, Mbeya na Dodoma.
Kamanda Kamwela alisema pia wamegundua kuwa watoto walikuwa wakiishi kwenye mazingira magumu ikiwamo kulala chini katika chumba kidogo.
Alisema polisi linawashikilia watu wawili (mume na mke) ambao wanatuhumiwa kuwahifadhi watoto hao.
Kamanda huyo alisema watoto hao wana umri wa kwenda shule, lakini walikuwa hawasomi.
Alisema polisi wanachunguza aina ya masomo ya dini waliyokuwa wakifundishwa.
“Lazima tuchunguze uhalali wa masomo ya dini waliyokuwa wakisoma ili tujue kama kweli watoto hawa walipelekwa na wazazi wao au la, kwa kuwa watoto hao walipaswa kuwa shuleni” alisema Kamanda Kamwela.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga alisema watoto hao walikuwa wakiishi kwenye mazingira magumu, huku wakipewa adhabu kali ikiwamo kubeba matofali mgongoni pindi wanapokosea.
“Maelezo ya watoto yanaonyesha walikuwa wakiteswa, adhabu hizi kwa watoto ni kubwa, bado tunawachunguza ili tujue kila kitu na walichukuliwaje huko majumbani kwao,” alisema Makunga.
Alisema kwa wazazi watakaowatambua watoto wao, wanapaswa kwenda na uthibitisho ikiwamo cheti cha kuzaliwa au uthibitisho mwingine utakaoonyesha ni mzazi halisi.
Maoni
Chapisha Maoni