Ufisadi wa kutisha waibuliwa

Dar es Salaam. Machungu ya Watanzania yakiwa hayajapoa kutokana na kashfa ya Sh306 bilioni kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ufisadi mwingine wa zaidi ya Sh252 bilioni umeibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ndani ya wizara ya ujenzi.
Ukaguzi maalumu uliofanywa na ofisi ya CAG katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11 na 2011/12 umebaini kuwa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, bungeni Novemba 2013 kuwa fedha hizo zilitumika kwa miradi ya ujenzi wa barabara, haikuwa sahihi.
Kutokana na ufisadi huo, habari zilizolifikia Mwananchi zinasema CAG amependekeza hatua stahiki zichukuliwe kwa wahusika wa wizara ya ujenzi na wakala wa barabara ili kuleta imani na uwazi katika bajeti kwa jamii na wahisani.
“Wizara (ya ujenzi) ililidanganya Bunge kuwa kuna ujenzi wa barabara hizo wakati wakijua kwamba walikusudia kulipa madeni ya wakandarasi na washauri wa ujenzi wa barabara...mpango mkakati wa wakala wa barabara wa mwaka wa fedha 2011/12 pamoja na manunuzi ulioidhinishwa havikuonyesha utekelezaji wa mradi huo,” chanzo cha habari kilikariri ripoti ya CAG.
Matumizi hayo yasiyo sahihi yaliibuliwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) Novemba 22, 2013 baada ya kutilia shaka kiasi hicho cha fedha na ofisi ya CAG kuagizwa kufanya ukaguzi.
Katika kikao hicho ambacho wizara ya ujenzi iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake wa wakati huo, Balozi Herbert Mrango alihojiwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe kuhusu hati ya mashaka waliyoipata kutoka kwa CAG mwaka 2011/12.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kwenye Bajeti ya mwaka huo Sh348.1 bilioni zilizokuwa zimetengwa chini ya fungu lililokuwa limetajwa kuwa ni la mradi maalumu hazikutumiwa kwa malengo yaliyoelezwa bungeni.
“Ni vizuri leo (ilikuwa Novemba 22 mwaka 2013) uiambie kamati fedha hizi ziliombwa kwa kitu gani na zilitumika kwa jambo gani. Tunajua kwamba fedha hizi zilipunguzwa Sh95 bilioni na kupelekwa Wizara ya Uchukuzi, zilibakia Sh252.975 bilioni katika kifungu hicho lakini kuna bilioni 100 zimetumika visivyo,” alisema Zitto.
Alisema katika majumuisho ya bajeti wizara hiyo, Dk Magufuli na Dk Harrison Makyembe aliyekuwa Naibu waziri wa wakati huo aliyekuwa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi walitoa maelezo yasiyo ya kweli bungeni kuhusu fedha hizo.
Zitto alikariri maneno yaliyorekodiwa kwenye Hansard ya Bunge yaliyosemwa na viongozi hao watatu.
“Tunaomba fedha Sh252 bilioni kwa ajili ya kuanzia kazi za ujenzi wa barabara.”
“Fedha hizi zitachangia miradi ya wafadhili,” haya yalikuwa maneno ya Dk Makyembe ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati akifafanua majumuisho.
Waziri wa Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli akikagua ujenzi wa kituo cha Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (BRT) Morocco jijini Dar es Salaam siku za hivi karibuni. Picha na Maktaba 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji