UANDIKISHWAJI: Usugu wa vidole kwa BVR watatuliwa

Makambako/Mwanza. Tatizo la watu wenye vidole sugu ambao awali vilishindwa kusomwa na mashine zinazotumika kuandikisha wapigakura za Biometrick Voters Registration (BVR) limepatiwa ufumbuzi na wataalamu wa mashine hizo walioambatana na tume katika mji huu kwa ajili ya kazi hiyo.
Watu hao walipatwa na mshtuko baada ya mashine hizo zinazofanya kazi kwa mara ya kwanza nchini kushindwa kutambua vidole vyao na kuwa katika hatari ya kukosa vitambulisho vitakavyowapa haki ya kupiga kura ya maoni kupitisha Katiba Mpya na ile ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Julius  Malaba aliliambia gazeti hili juzi kuwa, changamoto zote ikiwamo ya mashine za BVR kushindwa kusoma vidole vyenye usugu limetatuliwa, huku akisita kueleza namna lilivyotatuliwa.
“Pita katika vituo uone kama kuna mtu anarudiwa kwa tatizo la mashine kushindwa kusoma vidole vyake...,” alisema Malaba.
Gazeti hili lilipita katika vituo vya Bwawani, Ndondole, Lupila, Kitis, Lyamukena na vinginevyo kuuliza kama tatizo hilo lipo lakini wengi walikiri kuwa kwa sasa halijajitokeza. Mmoja wa watu waliokuwa na vidole sugu, Hardson Kinami aliliambia gazeti hili kuwa, mara baada ya kuingia katika chumba cha kuandikisha na kuchukuliwa maelezo mashine iligoma kusoma vidole vyake kwa zaidi ya mara mbili hali iliyompa hofu ya kukosa kitambulisho.
“Nilipata hofu kwani nimekuja jana (juzi) na kushindwa kuandikisha (leo) jana nimejihimu saa 10.00 alfajiri na nilipoingia ndani, mashine ikagoma kwa kweli nilishtuka sana...maofisa waliniambia ninawe mikononi na kusugua sehemu za vidole vitakavyogusa mashine, baada ya kufanya hivyo walinipa mafuta fulani na kuniambia niyafikiche ndipo mashine iliposoma vidole vyangu,” alisema.
Mtaalamu wa mashine hizo ambaye hakutaka jina lake litajwa kwa madai yeye si msemaji wa tume alisema, kilichotumika kutatua changamoto hiyo ni utundu tu na wala hapakuwa na njia ya kitaalamu ya kuitatua.
Akizungumzia changamoto ya mashine kuharibika alisema: “Kwa kawaida mashine hizi hazitakiwi kufanya kazi kwa muda mrefu, zinatakiwa kupumzishwa na kufanyiwa matengenezo, kwa hali hiyo ndiyo inatafsiriwa kuwa mashine zimeharibika,” alisema.
Hadi kufikia juzi, tume hiyo ilikuwa imeandikisha wapiga kura 19,396 na kazi hiyo ilikuwa bado inakabiliwa na changamoto ya wingi wa watu vituoni kiasi cha kusababisha vurugu kutokea kwa baadhi ya vituo.
Gazeti hili lilitembelea katika vituo vya Makatani ambako kulishuhudiwa mafundi waliopiga kambi Makambako wakiendelea na kazi ya kufanyia matengenezo mashine hizo.  Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva aliliambia gazeti hili kuwa changamoto zote zilizokuwa zikikabili kazi hiyo ikiwamo ya mashine kuharibika pamoja na vidole sugu zimetatuliwa.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema uandikishwaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa BVR hauwezi kukamilika wala kuwafikia Watanzania wote kwa wakati kwa wanaohitaji kuandikishwa na kudai kuwa ni wazi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imepanga kuharibu matokeo ya uchaguzi mkuu ujao.
 Pia, Mbowe alisema Serikali inakimbilia kujibebesha mizigo mizito ambayo haiwezi kuikamilisha kwa pamoja huku akitaja mizigo hiyo kuwa ni pamoja na Uchaguzi Mkuu ujao, kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji