Bilioni 103 za benki ya dunia kujenga nyumba

Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imetoa Dola 60 milioni (Sh 103 bilioni) za Marekani kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa wananchi.
Taarifa iliyotolewa na benki hiyo, ilieleza kuwa fedha hizo zitasaidia kuendeleza mradi wa ujenzi wa nyumba ulioanzishwa mwaka 2010 na kwamba kwa sasa thamani ya uwekezaji katika mradi huo imefikia Dola 100 milioni za Marekani.
Mkurugenzi wa Benki hiyo Tanzania, Burundi na Uganda, Phillipe Dongier alisema, ukuaji wa kasi wa miji unaonyesha kwamba kuna haja ya kuwapo kwa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
“Miji inakua kwa kasi, hivyo tunapaswa kutengeneza mazingira ya kutoa mikopo ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa wananchi.”
Pia alisema: “Lengo letu ni kusaidia upatikanaji wa nyumba za bei nafuu, mpango huu utazisaidia familia zenye kipato cha chini kumiliki nyumba na kuepuka gharama za kupanga.”
Dongier alisema fedha hizo zitasaidia upatikanaji wa mikopo nafuu na familia kumiliki nyumba zao badala ya kujenga nyumba kwa muda mrefu.
Mkurugenzi huyo alisema mpango huo utazivutia benki nyingine kutoa mikopo ya ujenzi kwa wakati tofauti kutokana na sasa mikopo ya nyumba kutopatikana kirahisi.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha, Dk Eliamani Sedoyeka alisema, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki ambazo uchumi wake unakua kwa kasi hivyo nyumba hizo zitasaidia uboreshaji wa makazi ya mijini.
Kwa upande wake, Mtaalamu Mwandamizi wa Kitengo cha Fedha kutoka Benki ya Dunia, Yoko Doi ambaye pia ni mjumbe wa Kikosi Kazi cha Viongozi wa Benki ya Dunia alisema, idadi ya benki zinazotoa mikopo ya nyumba imeongezeka kutoka nane mwaka 2010 hadi 19 kwa 2014 na muda wa kurejesha mikopo ya nyumba umeongezeka kutoka miaka saba ya awali hadi miaka 20 ambayo benki zinatoa kwa sasa.
Alisema wanaamini mchango huo wa IDA utaiwezesha TMRC kuwa imara ili kufanikisha malengo yake, ikiwamo kutumia fursa zilizopo kupanua wigo zaidi.
Tanzania Mortgage Refinancing Company (TMRC) ni kampuni ambayo inatimiza majukumu yake ya kuratibu na kuendeleza soko la nyumba za mikopo nafuu.
International Development Association (IDA) chini ya Benki ya Dunia imekuwa ikisaidia kundeleza makazi ya watu kwa gharama nafuu kwa kushirikiana na kampuni mbalimbali zinazohusika na miradi ya nyumba za bei nafuu.    

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji