Polisi watanda Muhimbili kuwazuia ‘JKT
Dar es Salaam. Polisi wenye silaha na mabomu ya machozi pamoja na maofisa usalama, jana walitanda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kuzuia vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wasimwone mwenyekiti wao, George Mgoba, aliyelazwa baada ya kutekwa na kuteswa na watu wasiojulikana.
Pamoja na hatua hiyo vijana wengine watatu akiwamo katibu wa wahitimu hao walikamatwa na polisi na walikuwa wanashikiliwa katika Kituo Kikuu jijini Dar es Salaam.
Mgoba Jumatatu iliyopita alitekwa, kuteswa na baadaye kutupwa kichakani katika eneo la Picha ya Ndege, Kibaha mkoani Pwani.
Kabla ya kufikishwa kwenye Hospitali ya Muhimbili, Mgoba alilazwa kwenye hospitali ya Tumbi Kibaha na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Amana wilayani Ilala.
Jana, wahitimu hao wa JKT wanaokadiriwa kufikia 200 walifika katika lango la Hospitali ya Muhimbili saa 11.50 asubuhi na kujichanganya na watu wengine waliokuwa wakisubiri kuwaona wagonjwa wao.
Ilipofika saa 12.10 magari ya polisi matano kila moja likiwa na askari sita yalifika katika eneo hilo na kuingia ndani ya eneo la hospitali hiyo huku polisi waliovaa sare wakisimama kwenye lango hilo kulinda usalama.
Makachero wengine waliingia ndani na kwenda moja kwa moja kwenye jengo la Mwaisela, wodi namba sita ambako Mgoba amelazwa.
Ilipofika saa 7.00 mchana watu waliofika kuangalia wagonjwa waliruhusiwa kuingia ndani na baadhi ya wahitimu wachache walijichanganya kwenda kuangalia wagonjwa.
Wengine wakamatwa
Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye na kuthibitishwa na Kiwango zilisema kuwa aliyekamatwa ni katibu wa wahitimu hao, Linus Emmanuel na wenzake wawili, ambao walitiwa mbaroni wakati wakienda Muhimbili na wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi.
Maoni
Chapisha Maoni