Pinda ammwagia sifa Peter Msigwa
Iringa. Waziri Mkuu Mizengo Pinda amemwagia sifa mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, akisema amekuwa kiongozi wa kwanza kuchangia vitanda 30 katika Hospitali ya Frelimo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Mchungaji Msigwa alimiminiwa pongezi hizo jana mchana wakati Waziri Pinda alipotembelea hospitali hiyo na kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali.
Kauli hiyo ya Pinda, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, kupongeza utendaji kazi mzuri wa viongozi wanaotoka vyama vya upinzani ni nadra sana kutolewa na viongozi wa chama hicho tawala.
Februari 10 mwaka huu Rais Jakaya Kikwete pia alimpongeza meya wa Manispaa ya Moshi (Chadema), Jaffar Michael kwa kile alichosema ni kusimamia vizuri na kutekeleza Ilani ya CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo.
“Nakupongeza kwa jitihada ulizozionyesha. Kitendo ulichokifanya kinatakiwa kuigwa na wadau wengine kwa sababu hospitali hii ina changamoto nyingi, “alisema Pinda.
Pinda alitaja changamoto hiyo kuwa ni kukosekana kwa vifaa vya upasuaji na hivyo kulazimika kuazima kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, na kutokuwa na eneo maalumu la kufua nguo na kulazimika kwenda hospitali hiyo ya rufaa.
Awali mganga mkuu wa manispaa hiyo Alexander Meya alisema Frelimo haina jengo la uchunguzi, utakasaji vyombo, sehemu ya kufulia nguo, chumba cha kuhifadhia maiti, gari la kubeba wagonjwa wala vifaa tiba.
Akijibu suala hilo, Waziri Pinda alisema kila kata inatakiwa iwe na kituo cha afya na kwamba bila manispaa husika kujua changamoto inazoikabili itaendelea kukumbwa na changamoto nyingi katika sekta ya afya.
Maoni
Chapisha Maoni