Tanzania tuitakayo na njia ya kuifikia
Kwa Wenyeviti wa vyama vyote vya Siasa hapa Nchini
Ccm, Chadema, Nccr Mageuzi, Cuf Udp, na vinginevyo
Ndugu
zangu, na viongozi wangu
Yah: Tanzania
tuitakayo na njia ya kuifikia
Ninajisikia
vyema kuwaletea waraka huu nikiwa na matumaini kuwa mtausoma kwa makini na
kuupa uzito unaostahili na ikibidi kuufanyia kazi kama kila mmoja wenu
atakavyoona na/au kwa pamoja kama ninavyopendekeza bila kujali umetoka wapi kwa
sababu mimi ni raia wa kawaida asiye na jina linalojulikana, Tanzania.
1.0 Utangulizi
Sasa
hivi Tanzania iko katika mchakato wa kuandika Katiba mpya. Japo hatujajua Watanzania
watapata katiba ya namna gani lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba tutapata
katiba mpya. Matumaini ya wengi ni kuwa Katiba hiyo itaweza kutoa mwelekeo wa
kutatua matatizo na changamoto ambazo zimejitokeza hivi karibuni na pia
kuelekeza Taifa hili liweje siku za usoni.
2.0 Mazingira tuliyomo.
2.1 Tunaweza kuyasoma mazingira tuliyomo kwa
namna mbali mbali. Mimi ningependa kujadili mazingira tuliyomo kwa kuzingatia jambo
hili: Ujirani na mataifa mengine na hali
ya siasa katika eneo letu hili sasa na mbele tuendako: Nafasi ya Tanzania
katika ushawishi wa kisiasa, kiuchumi hata kiusalama katika eneo letu.
2.2 Kwa muda toka tumepata uhuru Tanzania
imekuwa na mchango mkubwa wa kuyasaidia mataifa yaliyotuzunguka kujipatia uhuru
wao. Nchi zote zimepata uhuru angalau wa bendera. Ukiziangalia nchi zinazotuzunguka
licha ya kwamba nasi bado tuna matatizo ya demokrasia yetu, lakini naweza
kusema kwa ujasiri kuwa Tanzania ina utulivu wa kisiasa kuliko majirani zetu.
Tumeweza kubadilishana viongozi wa Juu bila mikwaruzo mikubwa, angalau hatujawahi
kulazimika kusuluhishwa kutoka nje. Si kwamba tunaridhika na kila kitu lakini
angalau si kama majirani zetu.
2.3 Tukiyapima mataifa yanayotuzunguka
unaona nchi nyingi zina migogoro au zina uwezekano mkubwa wa kuibuka migogoro
na hata kupigana. Nchi zinazotuzunguka zina vikundi vilivyo na silaha na
wengine hawataki hata kusuluhishwa, kwa hiyo kuna uwezekano wa kuendelea na
migogoro. Katika mazingira kama haya eneo linahitaji nchi ambayo majirani
wanaweza kuiheshimu, kuikimbilia kuomba msaada wa kutatua matatizo yake, lakini
hata kuiogopa kidogo (Regional Power).
Ukiuliza
mtu yeyote atakwambia ni Tanzania yenye uwezo wa kuwa hivyo. Na mimi nawaza
hivyo.
2.4 Lakini nikiiangalia Tanzania naona licha
ya kuwa ndilo taifa pekee linaloweza kukimbiliwa na majirani zake lakini sioni
kama lina uwezo kamili wa kufanya hivyo.
2.5 Nawaza kuwa ili taifa liweze kuwa
kamili na tayari kufanya hivyo lazima liwe na mambo makubwa manne:
- Liwe na Demokrasia nzuri.
- Liwe na Uchumi imara,
- Liwe na Jeshi imara na
- Liwe na Usalama wa Taifa imara.
2.6 Mimi siamini kuwa haya manne tuko imara
kiasi cha kuwaangalia majirani wakatuheshimu. Kumekuwa na migogoro na mijadala
na majirani zetu wa Malawi na Rwanda. Nimeshiriki kujadili habari hizi kupitia
mitandao ya jamii hasa Wanabidii. Ninaamini kama balaa lingeingia tukaingia
vitani na mmoja wa majirani hawa, Tanzania tungeshinda vita hiyo. Lakini ukweli
tungeingia vitani. Ninaposema kuwa na jeshi imara nina maana kuwa na jeshi
ambalo nchi jirani zinaogopa kupigana nalo hivyo hawawezi kuwa wa kwanza
kutuchokoza kwa kuwa wanaogopa.
2.6.1 Demokrasia:
Hata
kama Tanzania inayo demokrasia lakini malalamiko na mahusiano ya wanasiasa wetu
ni ya kimaslahi zaidi kuliko kujenga nchi. Ukiangalia utakuta watanzania hatuna
kitu kinachotuunganisha. Hatuna lengo la kiuchumi ambalo kila Chama cha siasa
kinajieleza kitalitimizaje. Sikukuu za kitaifa hazituunganishi. Nadra kuwakuta
viongozi wetu wa vyama vya siasa mmekutana katika siku hizi au siku nyingine mmeitana
kushauriana juu ya jambo fulani la kitaifa. Katika ziara za kikazi viongozi
wetu wa serikali hukosi alama za vyama vya siasa au matamshi ya kukejeliana.
Hii sio maana hasa ya siasa tunayoitamani. Tunahitaji kujenga demokrasia ya
kweli ambayo tutapingana katika mambo ya msingi na kukubaliana katika mambo ya
msingi. Ninaamini tunaweza kuwa na demokrasia ambayo tunatofautiana mbinu ya
kutimiza malengo yetu.
Ninakumbuka
wakati taifa la Israel lilipotuma askari wake kuwakomboa wenzao waliokuwa
wametekwa na kuletwa Entebe Uganda, waziri mkuu wa Israel alimtaarifu kiongozi
wa upinzani kwanza. Walibishana kwanza na baadaye wakakubaliana na ndiye
aliyekuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya operation hiyo.
Tanzania
kwa mazingira tuliyo nayo tunahitaji siasa hizo zaidi. Sasa tumegawanyika
kiitikadi kiasi badala ya siasa kutuunganisha inatutenganisha. Hii inaweza
kulipeleka taifa pabaya achilia mbali kulizuia kwenda mbele.
2.6.2 Uchumi:
Tanzania
ina nafasi nzuri za kujenga uchumi wake na wananchi wake wakaondokana na
umaskini. Nitataja maeneo ninayoyaona kuwa yanaweza kuliendeleza taifa hili
kila moja likiwa peke yake:
a) Bandari, na reli.
Tanzania ina eneo kubwa la bahari. Ninaamini kama Tanzania ikijenga bandari za
kisasa tatu tu Tanga, Dar Es Salaam na Mtwara; Ikaimarisha reli za kati na
Tazara inaweza kuwahudumia nchi jirani zisizo na mlango wa bahari, na kukusanya
mapato ya kutosha kuendesha nchi hii bila misaada wala mikopo mikubwa kutoka
ndani na nje. Tunahitaji kuweka misingi ndani katiba zetu na mifumo yetu ya
uongozi zitakaotusaidia hata kuchagua rafiki. Kuna nchi zina bandari nzuri na
tunaweza ama kuiga kwao au kwenda kujifunza kwao na tukajenga zetu.
b) Madini na gesi asilia:
Wote tutakumbuka kuwa nchi kama Libya wakati wa Ghadafi wananchi wake
walineemeka na raslimali mafuta. Kama tukiweka kwenye katiba yetu namna nzuri
ya kuwanufaisha watanzania tunaweza kujikuta hatulazimiki kutoza wananchi wetu
kodi kubwa kwa sababu ya kiburi cha utajili huo wa madini na gesi.
c) Ardhi yenye rutuba:
Tanzania ni nchi iliyoneemeka kuwa na ardhi inayoweza kulimika. Kama Tanzania
ikipunguza eneo linalolimwa na mkulima mdogo mdogo, na eneo litakalolimwa
likalimwa kisasa (intensive farming), mazao yatakayolimwa yatatosheleza
mahitaji ya ndani na kuuza ziada nje na eneo kubwa likabaki kwa ajili ya mifugo
na kupanda misitu hivyo kulinda mazingira. Niliwahi kufanya utafiti na kugundua
kuwa kilimo bora cha migomba ekari moja inatosheleza mahitaji ya chakula kwa
familia kumi na moja.
Maana
yake kama kilimo kikisimamiwa; badala ya 80% ya watanzania kuwa ‘wakulima’
watapungua hadi 20% na hao watalisha nchi nzima na kuuza ziada nje bila
kulazimika kuwaita wakulima wakubwa kutoka nje. Faida yake ni kuwa:
i)
Eneo dogo tutajilisha na kulisha jirani
zetu.
ii)
Maeneo yaliyobaki tutatenga kwa ajili ya
mifugo
iii)
Na maeneo mengine yatabaki kustawisha
mazingira kwa kuoteza misitu na kuweka kwa kilimo cha baadaye.
d) Utalii: Tuna
vyanzo vingi vivutio vya utalii. Maziwa, Mbuga nakadhalika. Tukiwekeza katika maeneo hayo Tanzania itajenga uchumi wake na
wananchi wake na hivyo kupunguza kutegemea misaada. Kilimo na utalii
vinawezekana bila misaada kutoka nje.
2.6.3 Jeshi na usalama wa Taifa:
Kama
tukiwa na demokrasia ya kweli na uchumi mzuri Tutalazimika kujenga vyombo hivi
viwili na wala hakuna nchi inayoweza kutushtukia. Tutakuwa na uwezo na sababu.
Uimara wa jeshi unaweza kutatua migogoro ya jirani zetu si kwa kuwalazimisha
lakini kwa kuwashauri na pengine kuwabana watende haki kwa raia wake.
Nikiangalia mazingira ya nchi ya Syria; kama si uwezo wa kijeshi wa nchi za
magharibi huenda Syria isingesalimisha silaha za sumu. Tanzania tuliisaidia
nchi ya Comoro kuukomesha uasi uliojitokeza. Msaada uliotolewa Comoro kutoka
Tanzania hatuwezi kuutoa Kenya mambo yakibadilika. Tuna nafasi ya kuwa na uchumi
imara kuliko majirani zetu na hivyo kujenga ulinzi wetu kwa manifaa yetu na
jirani zetu.
3.0 Mchakato:
Tanzania
inahitaji kuandaa vision yake katika kujenga taifa kama nilivyolieleza (au hata
la namna nyingine). Na baada ya kuiandaa vision hiyo tunahitaji kuwa na mfumo
wa kuiendesha kupitia vyama vingi. Ni vizuri kujifunza kwa mataifa mengine;
yaliyoendelea na yanayoendelea. Kitu kimoja nafikiri ni muhimu ni kuwa lazima
vision hiyo iandaliwe na watanzania wote bila kujali tofauti zao kiimani,
kieneo (hasa eneo la Muungano) na kiitikadi pia. Na hasa kuweka mpango ambao
unaweka mipaka ya itikadi. Tuwe na tunu za kitaifa na namna ya kuziendesha.
Mathalan tukisema sikukuu za kitaifa watu wote wanajumuika hatutegemei kuwakuta
wenzetu wa chama fulani hawapo kwa vyovyote vile.
Ili
kujenga mfumo huo tunahitaji kuwa na kipindi cha mpito. Kipindi ambacho tutakitumia
kufanya maamuzi kama waTanzania na hata kupanga mipaka hiyo ya itikadi zetu.
Ili
kufikia hapo tunahitaji mambo mawili:
1=
Kuwa na kipindi cha uongozi wa Mpito ambamo licha ya vyama vyetu kuendelea
kufanya kazi zake kama kawaida lakini kipindi hicho kisigubikwe na mkanganyiko
wa kiitikadi kama sasa.
2=Kipindi
hicho kuongozwa na Rais ambaye tumemkubali kama watanzania kukiongoza. Rais
huyo aonekane kuwa na sifa zifuatazo:
- Muumini wa dini lakini asiye na ‘udini’.
- Mzanzibari (au Mtanganyika) asiye na Uzanzibari (au Utanganyika), bali yeye Uzanzibari wake una maana kama utanganyika kwa manufaa ya Muungano.
- Mwanachama wa chama cha siasa asiyetawaliwa na Itikadi za chama chake, bali anautanguliza utanzania mbele.
Kiongozi
huyo aliongoze Taifa kwa kipindi cha miaka mitano na moja kati ya kazi zake ni
kuwaunganisha watanzania na kuwaandaa kufanyika uchaguzi wa vyama vingi katika
mfumo wa kuheshimu malengo ya taifa. Alisaidie Taifa katika kipindi hicho
kujenga misingi ya UTAIFA kwa vitendo.
4.0 Manufaa ya mpango huu
Mpango
huu una manufaa makubwa sana.
1 Kwanza hebu tukubali kuwa
tumetingishika kidogo. Taifa limeshuhudia mambo fulani yaliyojitokeza na kuonyesha
kugawanyika.
2 Pili hebu tukubali kuwa kila kundi
linaona linaweza kutatua matatizo tuliyo nayo. Na kila kundi linataka kufanya
hivyo kulishinda kundi jingine. Hii ni nzuri kama ni jambo la kawaida. Lakini
kunapokuwa hata na amani inatishiwa, ni ngumu kufanikisha. Kwa hiyo kuwa na
serikali inayoungwa na wote ambamo mafanikio yake hayatamnufaisha mmoja wapo,
ni mpango mzuri.
3 Lakini manufaa mengine ni kule kuamua
wenyewe kuwa na uongozi wa Mpito. Karibuni Zimbabwe ilikuwa na uongozi wa
pamoja. Kenya vile vile. Maamuzi yalitoka nje ya nchi hizo. Kwa hiyo sisi kuona
hivyo na tukasema tunapumuzisha itikadi zetu katika uongozi wa miaka mitano ili
kukamilisha mambo fulani mataifa yote yataishangaa na kuipongeza Tanzania.
Licha ya kuwa sifa nyingi zinaweza kuiendea serikali iliyopo madarakani lakini
vyama vyote kuunga mkono mpango huu katika uchaguzi ni sifa kwa taifa zima.
4 Manufaa ya nne baada ya hapo Tanzania
itakuwa imara na sifa zake zilizolegea baada ya rais wa awamu ya kwanza
zitarudi pale pale.
5 Manufaa mengine ni kupata mwanzo mzuri
wa uendeshaji wa nchi baada ya katiba mpya ambomo moja kati ya mabadiliko
yanayotarajiwa ni Nchi kuwa na Serikali tatu.
5.0 Mapendekezo:
Naomba
kujitetea kuwa mimi si mwanasiasa na si mzoefu wa miundo ya serikali. Lakini
nina mapendekezo yanayoweza kurekebishwa katika mchakato kama inavyoweza
kuonekana inafaa.
1) Rais.
Napendekeza
mtu ninayemuwazia kuongoza serikali hii kuwa ni Salim Ahmed Salim
Akikubaliwa
ataunda serikali kwa uhuru kamili kwa mujibu wa katiba iliyopo/itakayokuwepo na
hatalazimika kuchagua mawaziri wake kutoka chama chake bali atakavyoona inafaa
2) Bunge
Bunge
litachaguliwa kutokana na wagombea wa vyama vya siasa kwa mujibu wa katiba
iliyoko/itakayokuwapo, isipokuwa Chama Cha mapinduzi hakitatumia Jina la Salim
kuwanadi wabunge wake.
3 Ili kuhakikisha hili linafaya kazi
wakati wa kampeni ya Rais kutakuwa na wawakilishi wa vyama vyenu
nilivyoviandikia na vingine vinavyounga mpango huu/mgombea huyu mkono. Vyama
ambavyo havitakubaliana na mpango huu vitakuwa vimesimamisha wagombea urais wake.
Ikitokea vyama vyote vikauunga mkono basi kura ya Rais itakuwa ya ndiyo na
hapano.
Napendekeza
kwenu kuwa kama mpango huu utakubaliwa basi Rais Kikwete aitishe kikao cha
faragha kuujadili nami nikaribishwe katika kikao hicho ili kujieleza kama kuna
mahala sijaeleweka lakini na kuweka mawazo yanayoweza kuwa yamebaki bila
kujitokeza ndani ya waraka huu.
Ninapendekeza
pia kuwa Mpango huu ukikubalika MIMI ndiye niwakilishe pendekezo hili Kwa Salim
(au mtu mwingine anayeweza kuonekana anafaa). Sababu ni njema ili kumuonyesha
kuwa wazo lilikotoka mahala fulani.na hkama hii itawakilisha maslahi ya vyama
vyote vinavyoshiriki.
Natanguliza
shukrani zangu za dhati kwa uaminifu wenu kwa taifa hili si kwa kuyaheshimu
mawazo haya ninayoyatoa bali na kazi nyingine mnazoonekana kuzifanya katika
mfumo huu wa vyama vingi.
Ndimi
mtanzania mwenzenu
Maoni
Chapisha Maoni