Dk Hoseah awanyatia wagombea urais CCM

Dar es Salaam. Wakati viongozi wajuu wa CCM wakiendelea kulalamikia makada wanaowatuhumu kutumia fedha kujifagilia njia ya urais, mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah amesema taasisi yake inakusanya taarifa zote za wanachama wa chama hicho tawala wanaotuhumiwa kutumia mlungula.
Mara kadhaa viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakiwaonya wanachama wao dhidi ya makada wanaotumia fedha kujitengenezea mazingira mazuri ya kupitishwa na chama hicho kugombea urais, lakini wameeleza kuwa hawawajibiki kuwaripoti Takukuru kwa kuwa ni wajibu wa chombo hicho cha kuzuia na kupambana na rushwa kufanyia kazi malalamiko hayo.
Jumatano, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alisema Takukuru hawahitaji kupata mwaliko wa CCM ili kufanya uchunguzi wa kukamata wagombea wanaotumia rushwa ndani ya chama hicho kwani rushwa inayoendelea kwa sasa iko wazi.
“Kazi ya kuwafuatilia imeshaanza muda mrefu, tunazo taarifa zao za kutosha kwa kila mwanasiasa anayelalamikiwa,” alisema Dk Hoseah wakati alipoongea na gazeti hili kuhusu sababu za taasisi yake kukaa kimya wakati ikielezwa hadharani kuwa rushwa imezidi katika harakati za uchaguzi ndani ya CCM
Dk Hoseah alisema kwa muda mrefu Takukuru imekuwa ikifuatilia mienendo ya wanasiasa wanaotaka uongozi kupitia chama hicho na ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema Takukuru kwa sasa inaendelea na kazi yake ya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo huku ikikusanya taarifa za kila mwanasiasa anayeonekana kutuhumiwa na vitendo vya rushwa.
“Siyo kwamba Takukuru haijaona wala haisikii malalamiko ya viongozi CCM. Tunajua wajibu wetu na kazi ya kuwafuatilia imeshaanza,” alisema Dk Hoseah.
“Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 imekataza wazi kwamba, ni makosa kutoa chochote kama zawadi kwa kundi la watu, vinginevyo ni kukiuka sheria hiyo. Labda kama anaonekana kuwa na fedha nyingi basi ajenge hata barabara kuliko kufanya hivyo.”
Dk Hoseah aliongeza kuwa sheria pia inazuia kuanza kampeni kabla ya muda kupangwa rasmi na Tume ya Taifa (Nec), kwa hivyo muda wa kampeni utakapoanza, itarahisisha kukusanya taarifa zake na kuchukua hatua kwa wanasiasa hao.
“Kwanza ni kosa kufanya kampeni kabla ya muda, lakini pia ni kosa kutoa zawadi kama maji ya kunywa kama unafahamu kuwa wewe ni mwanasiasa utakayegombea. Sheria yetu ya Takukuru inaweka wazi pia kitendo hicho ni kosa,” alisema Dk Hoseah.
Mapema wiki hii, akiwa kwenye vikao vya ndani na viongozi wa chama hicho wa Dar es Salaam, makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangulla alisema fedha zinazotumiwa na makada kununua wanachama “kama maandazi”, zitakuwa kitanzi chao kwenye uchaguzi mkuu, akisisitiza kuwa wanachama hao watang’olewa.
Mbali na Mangula, wengine waliowahi kulalamikia rushwa ndani ya chama hicho ni mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete ambaye alitahadharisha kuwa jambo hilo linaweza kukiuangusha chama.
Mkurugenzi wa Takukuru Dk Edward Hosea

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji