Dk Slaa atua Dar, arusha kombora zito

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kuandikisha wapigakura kwenye mikoa ambayo ni ngome ya CCM na kwamba ile yenye upinzani itaandikishwa kwa kulipua ili watu wengi wenye sifa ya kupiga kura wasiandikishwe.
NEC ilianza kuboresha Daftari la Wapigakura kwa kuandikisha wananchi wa Mkoa wa Njombe, ambako watu 300,080 waliandikishwa kati ya 392,634 waliotarajiwa na sasa inaelekea mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa baada ya kupokea mashine nyingine 1,600. Kazi hiyo itaendelea kwenye mikoa ya Katavi, Mbeya na Dodoma wakati mashine 1,600 zaidi zitakapowasili.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva amesema hilo ni jambo jipya kwake kwa kuwa hawakuangalia suala hilo wakati wa kupanga mikoa hiyo.
Akizungumza jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mara baada ya kuwasili nchini akitokea Marekani, Dk Slaa alisema wamegundua kwamba mwishoni mwa kazi ya uandikishaji kwenye mikoa ambayo ni ngome ya vyama vya upinzani, watu wengi hawataandikishwa.
“Tumegundua hujuma zao, NEC wameanza kuandikisha wapigakura kwenye mikoa ambayo ni ngome ya CCM. Huko wanajitahidi kuandikisha wapigakura wote na wanachukua muda mrefu,” alisema Dk Slaa akionekana kurejea Mkoa wa Njombe ambako NEC imetumia takriban miezi miwili kuandikisha wapigakura.
“Mikoa yenye ngome ya Chadema na vyama vingine vya upinzani itakuwa ya mwisho kuandikisha wapigakura na uandikishaji huo utakuwa wa harakaharaka ambao utawaacha mamia ya watu bila kuandikishwa kwa sababu muda utakuwa hautoshi,” alisema Dk Slaa.
Alisema suala hilo linaweza kuvuruga uchaguzi, hasa ikizingatiwa kwamba mchakato wa uandikishaji umekuwa na sintofahamu nyingi.
Kwa mujibu wa matokeo ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, CCM ilivuna kura 128,809 katika majimbo matatu ya mkoani Njombe (Njombe, Ludewa na Makete) wakati huo ukiwa ndani ya Mkoa wa Iringa. Chadema ilifuatia kwa kupata kura 36,928 na CUF/NCCR zilipata kura 1,670
Kwa kujumuisha kura hizo na majimbo mengine ya Iringa CCM ilipata jumla ya kura 299,799 ikifuatiwa na Chadema iliyopata kura 76,010. CUF na NCCR-Mageuzi zilipata jumla ya kura 3,137. Hadi sasa upinzani una mbunge mmoja tu kwenye mikoa hiyo miwili, Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini.
Kwenye uchaguzi wa Rais mwaka 2010 mkoani Lindi, mgombea wa CCM alipata kura 150,118 akiwa mbele ya mgombea wa CUF aliyepata kura 64,875 wakati wagombea wa Chadema na NCCR walipata jumla ya kura 12,880. Wapinzani wana wabunge wawili mkoani Lindi ambao ni Selemani Bungera wa Kilwa Kusini na Salum Barwany wa Lindi Mjini, wote kutoka CUF.
Mkoani Mtwara, mgombea urais wa CCM alipata kura 213,844 akimuacha mbali mgombea wa CUF aliyepata kura 81,953, huku wagombea wa Chadema na NCCR wakipata jumla ya kura 82,233. Hakuna mbunge kutoka upinzani mkoani Mtwara.


Takwimu za 2010 pia zinaonyesha kuwa mkoani Ruvuma, mgombea urais wa CCM alipata kura 198,090, akimuacha kwa mbali mgombea wa Chadema aliyepata kura 36,044, CUF (28,873) na NCCR kura 397.
Chanzo Mwananchi Gazeti

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji