Escrow yampa tuzo Kafulila

Dar es Salaam. Sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow limemng’arisha Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi),  David Kafulila baada ya kutunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kufichua ufisadi huo uliohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika sakata hilo, mawaziri wawili walipoteza nyadhifa zao pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuwahusisha na sakata hilo. Maofisa wengine kadhaa wa Serikali wamesimashwa au kufunguliwa mashtaka kutokana na kuhusika kwao kwenye ufisadi huo.
Sakata hilo lililoteka kwa kiasi kikubwa mkutano wa Bunge wa 16 na 17 kabla ya kufika bungeni,  liliibuliwa na Gazeti la The Citizen, linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd na Kafulila kuwasilisha hoja ndani ya Bunge ili kujadiliwa.
Tuzo aliyopewa Kafulila jana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu unaounganisha asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu (THIRD-Coalition), ni moja kati ya tuzo tatu zilizotolewa kwa Watanzania walioonyesha ujasiri katika kutetea haki za binadamu nchini.
Wengine ni Maanda Ngoifiko wa asasi ya kiraia, inayotetea haki za binadamu ya PWC kutoka  Loliondo  wilayani Ngorongoro, na Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Salma Said aliyetishiwa kuuawa baada ya kuonyesha msimamo wa kukataa shinikizo la kukubaliana na muundo wa Muungano wa serikali mbili wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.
Kwa mujibu wa THIRD-Coalition, vigezo vilivyotumika kuwapata washindi hao vilizingatia mazingira ya kazi na hali hatarishi aliyokutana nayo mshindi wa tuzo hiyo, ikiwamo taarifa zilizokusanywa kupitia ripoti za matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mwaka jana.
Baada ya kukabidhiwa, Kafulila alisema tuzo hiyo ni mwanzo wa hatua nyingine ya kuendelea kuibua ufisadi ndani ya Serikali.
“Nimepata ujasiri na kuamini kwamba siko peke yangu katika vita hii, nashukuru kupata tuzo hii, lakini nashukuru zaidi ushirikiano nilioupata kwa mhariri wa gazeti la The Citizen, ambaye alinipatia nyaraka nne za kuanzia,” alisema Kafulila.
“Hata hivyo, ninasikitishwa kuona bado Tanesco wakiendelea kulipia Dola 4 bilioni za capacity charge kwa kampuni hiyo ya ITPL, wakati hukumu iliyotolewa na Mahakama ya ICSID ya Uingereza Februari 12, mwaka jana inasema haikuwa sahihi tozo hiyo, lakini bado kiwango hicho kinaendelea kulipiwa.”
Salma alisema pamoja na vitisho ambavyo bado ameendelea kukutana navyo mpaka sasa kutoka kwa baadhi ya wabunge wa lililokuwa Bunge la Katiba, bado msimamo wake utaendelea kuwa palepale.
Aidha, alisema vita iliyopo kwa sasa imehamia kwenye harakati za Baraza la Katiba la Zanzibar ambalo linaendesha elimu kwa Wazanzibari kuhusu Katiba Inayopendekezwa. “Mimi ni mjumbe wa Baraza hilo na kwa sasa hawapendi kuona tukielimisha ukweli wa Katiba hiyo na badala yake wanataka kueleza mazuri tu. Hilo tumesema haliwezekani.”

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila akikabidhiwa Tuzo ya utetezi wa haki za binadamu ya mwaka 2014, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tom Nyanduga, Dar es Salaam jana.  Kulia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini, Martina Kabisama. Picha na Kelvin Matandiko 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji