Uamuzi huo wa Ccm haunisumbui; Bw, Moyo
Dar es Salaam. Aliyekuwa mwananchama namba saba wa CCM, Hassan Nassor Moyo amesema hana matatizo na uamuzi wa chama hicho kumvua uanachama kwa kuwa hakutarajia kama angezaliwa na kuwa mwanachama wa chama hicho.
Moyo, ambaye amewaelezea waliomtimua kuwa ni watoto wadogo, ameongeza kuwa pamoja na kutimuliwa hatarajii kujiunga na chama chochote cha siasa kwa kuwa ni mzee muda huu na anahitaji kupumzika. Akizungumza kwa simu na Mwananchi akiwa mkoani Tanga ambako amesema amekwenda kupumzika kwa siku 30, Moyo alisema anachokiona ni kuwa CCM ya sasa ni tofauti na Tanu na ASP vilivyokuwa vinakubali kukosolewa.
“Mimi nilikuwa ni mwanachama wa ASP, tulikuwa tukikosoa maamuzi mengi tu vikaoni na (rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani) Karume hakuwa akikasirika.
“Naambiwa kuwa nimekwenda kinyume na msimamo wa chama kwa kusema tuwe na muundo wa Muungano wa serikali tatu, kwani msimamo wa chama ni kuwa na Muungano wa serikali mbili. Hiyo si kweli, msimamo wa chama ulikuwa serikali mbili kuelekea moja, sasa mbona hawazungumzii serikali moja, hasa ukizingatia kuwa muundo wa serikali mbili ulikuwa ni wa mpito tu?” alihoji Mzee Moyo. Moyo, ambaye alikuwa waziri wa kwanza wa elimu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, amekuwa akiikosoa Serikali ya Zanzibar kwenye mikutano mbalimbali, ikiwamo anayoiitisha kuzungumzia masuala mbalimbali.
Alipinga bayana muundo wa serikali mbili na kusisitiza umuhimu wa Zanzibar kuwa na mamlaka kamili, mambo ambayo ni kinyume na msimamo wa Serikali ya CCM. Moyo amekuwa akizungumzia umuhimu wa kuandika Katiba mpya tangu mwaka 2009 na amekuwa akikiri kuwa Zanzibar iliukubali Muungano bila ya matatizo, na hata suala la gesi ambalo alisema liliingizwa mwaka 1968, lakini anasisitiza kuwa kama kuna kosa lilifanyika, vijana hawana budi kulihoji kwa kuwa walisomeshwa ili wapate ufahamu huo. Alipoulizwa kuhusu msimamo wake hivi sasa baada ya kufukuzwa na chama chake, Mzee Moyo alisema msimamo wake bado ni maridhiano.
“Mimi nilikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, CCM wanasema kamati hiyo hawaitambui, ni sawa kabisa kwani kamati ile haikuwa ya chama chochote kile, ilikuwa ni Kamati iliyoundwa na watu wenye nia njema ili kutafuta mwafaka wa kisiasa Zanzibar,” alisema.
“Kamati hiyo iliundwa baada ya Kamati Kuu ya CCM iliyoketi mjini Butiama na kuamua kuwa ipo haja ya kuwa na maridhiano Zanzibar ili kutuliza hali ya hewa ya kisiasa iliyokuwa ikichafuka kila uchao.
“Kwa kweli tulifanya kazi kubwa mpaka yakapatikana maridhiano ambayo ndiyo yaliyosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kusema kweli kazi tuliyofanya ni nzuri, kwani nchi imetulia, na hali hiyo mimi najivunia.”
Je, atajiunga na CUF?
Mwanasiasa huyo alisema ameshakuwa mtu mzima, hivi sasa anahitaji kupumzika na alishaacha siasa zamani hadi wenzake walipokwenda kumwomba aingie katika Kamati ya Maridhiano. “Sitaki kujiunga na chama chochote cha siasa, mimi ni mzee sasa, nahitaji kupumzika,” alisisitiza Mzee Moyo.
Kuhudhuria mikutano ya CUF
Maoni
Chapisha Maoni