Serikali yataja asasi 24 zitakazofutwa

Dar es Salaam. Serikali imeanza kutimiza ahadi yake ya kuyafuta mashirika na asasi zisizo za kiserikali, NGO, yakiwamo ya kidini na kwa kuanzia imetangaza kusudio la kuzifuta asasi 24 katika kipindi cha siku saba kuanzia jana.
Miongoni mwa asasi hizo ni taasisi mbili za dini ambazo ni Tanzania Muslim Social Community na Tanzania Christian Outreach Ministries ambazo zimepewa siku saba kujitetea.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Issack Nantanga aliliambia gazeti hili kuwa asasi zote zitakazothibitika kwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake, zitafutwa.
Nantanga pia alisema panga hilo litazipitia pia asasi ambazo zimekuwa haziwasilishi kwa msajili ada ya kila mwaka na taarifa za fedha zilizokaguliwa na wakaguzi waliosajiliwa.
“Haya mashirika 24 ndio tumeanza nayo na ukaguzi unaendelea. Tumetoa muda wa siku saba kuanzia leo (jana) kujitetea kwanini yasifutwe na wakishindwa kufanya hivyo, yatafutwa rasmi,” alisema.
Aliyataja mashirika mengine kuwa ni Kagwa Development Society, Morning Star Production Training Centre, Chama cha Kujitegemea na Kujiendeleza na The Organisation of Tanzania Community.
Mashirika mengine ni Mbezi Juu and Salasala Woman Agricultural and Environmen Association, Waridi Training Society, Vituka Machimbo Development Association na Gerezani Nguvukazi.
Mengine ni Nyakasangwe Small Scale Farmers Association, Vitendo Trust Fund, Bahari Beach Silvers and Woman Association, Owners Social Club na Magovent Development Association.
Kwa mujibu wa Nantanga, mashirika mengine yaliyomo katika orodha hiyo ni Hananasifu Quarters Women Association, Mburahati Barafu Development Community na The Movers Club.
Pia yamo Umoja wa Maendeleo ya Jamii Mlima Mindu, Tabata Tujiimarishe Club, Umoja wa Wauza Miche Ubungo, Kunguru/Kinzudi Development Association na Women & Environment Association.
“Ukitazama katika tovuti ya wizara utakuta tuna orodha ya mashirika 10,624 yaliyosajiliwa tangu 1953. Tutapitia moja baada ya jingine na yatakayobainika kukiuka sheria yatafutwa,” alisisitiza.
Wakati Serikali ikianza mchakato huo, imebainika kuwa baadhi ya klabu za waandishi wa habari za mikoa, nazo ziko hatarini kuangukiwa na rungu hilo kwa kutolipa ada. Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya klabu hizo za waandishi wa habari hazina taarifa za fedha zilizokaguliwa na wakaguzi waliosajiliwa na wala taarifa hizo haziwasilishwi kwa msajili.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji