Watanzania waliokuwa Afrika Kusini warudishwa

Dar es Salaam. Serikali imewarejesha nyumbani Watanzania 26 walioathiriwa na mashambulizi yanayofanywa na wazawa dhidi ya wageni katika Jiji la Durban nchini Afrika Kusini.
Habari za uhakika zilizopatikana jana Jijini Dar es Salaam, zilieleza kuwa Watanzania hao, walirejea nchini jana alfajiri na kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ndege ya Shirika la Precision Air.
Hata hivyo, jitihada za kumpata Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe hazikuzaa matunda lakini Naibu wake, Mahadhi Juma Maalim alithibitisha habari hizo.
“Ni kweli tumewarejesha Watanzania 26 waliwasili leo (jana) asubuhi kutoka Afrika Kusini na hii ilikuwa ni ahadi ya Serikali siku zote tunajali usalama wa raia wetu popote walipo,” alisema Maalim.
Hivi karibuni, Waziri Membe alisema kuwa Serikali ilikuwa na mpango wa kuwarudisha Watanzania hao baada ya kutokea machafuko hayo kwa wenyeji kuwapiga na kuwaua wageni kwa kile walichodai ‘kuwaminya’ kwenye ajira zao.
Habari zaidi zilisema Watanzania hao walisafiri kwa ndege kutoka Durban juzi usiku hadi Pretoria na usiku huo huo, wote wakafanikiwa kupata nafasi kwenye ndege ya Precision na kurejea nchini jana.
Wiki iliyopita, Membe alisema Watanzania 23 waliokuwa wamewekwa kwenye kambi maalumu ya Isipingo nchini Afrika Kusini ili kupewa ulinzi kutokana na mashambulizi yanayofanywa na wazawa.
Miongoni mwa Watanzania hao, 21 walikuwa wameridhia kurejea nyumbani na wanatarajia kuwasili nchini muda wowote lakini wengine wawili waliomba kuendelea kubaki nchini humo.
Membe alitumia mkutano huo kukanusha taarifa kuwa wapo Watanzania waliofariki nchini humo kutokana na vurugu hizo akisema watanzania waliofariki, walikufa kwa sababu mbalimbali.
Hata hivyo taarifa hizo zimekuwa zikipingwa kupitia baadhi ya Redio na mitandao ya kijamii hapa nchini, huku Redio moja ikimkariri mtanzania mmoja akidai alishuhudia watanzania wanne wakifa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benardb Membe. 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji