Ikulu: JK hajazuia kampeni, ni sheria
Dar es Salaam. Ikulu imesema kuwa Rais Jakaya
Kikwete hajazuia kufanyika kwa kampeni kuhusu Kura ya Maoni isipokuwa
Sheria ya Kura ya Maoni ndiyo inayozuia kufanyika kwa kampeni hizo kwa
sasa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Salvatory
Rweyemamu alisema hayo Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa sheria hiyo
inaelekeza kampeni kufanywa ndani ya siku 60 kabla ya kufanyika ya
kupiga kura ya maoni.
“Kimsingi Rais hajakataza kampeni, Sheria ya Kura
ya Maoni ndiyo inayokataza, lakini kinachofanyika ni kutoa elimu kama
inavyofanya Serikali, hiyo inaruhusiwa...Serikali haifanyi kampeni,
nasisitiza,” alisema.
Rweyemamu alisema hayo baada ya Rais Kikwete kuwahutubia Wazee wa Mkoa wa Dodoma, Jumapili iliyopita.
Alipoulizwa kuwa Ikulu inafanya kazi ya asasi za
kiraia zilizoainishwa kwa mujibu wa sheria kufanya kampeni za kuelimisha
umma kuhusu Kura ya Maoni, Rweyemamu alisema Ikulu inatoa somo la
uraia lakini si kupiga kampeni.
Alipotakiwa kueleza kama ni elimu, kwanini
inawataka Watanzania kupiga kura ya ndiyo, Rweyemamu alisema: “Tunatoa
civic education (elimu ya uraia) na hiyo ya kusema wapige kura ya
ndiyo, haikatazwi kwani wapi kuna sheria inayokataza Serikali kutoa
elimu?”
Hata hivyo, Rweyemamu alisema kuwa Serikali ndiyo yenye mchakato wa Katiba hivyo haikatazwi kupigia kampeni.
“Utakaaje kimya wakati watu wanapiga kampeni huko?
Sisi tumeingia mtaani baada ya wengine kufanya hivyo, japokuwa kuna
utaratibu wake,” alisema.
Kauli ya JK Dodoma
“Ninaomba Watanzania wenzangu tuzingatie mamlaka
ya Sheria ya Kura ya Maoni ambayo imeelekeza vizuri lini kura ya maoni
itapigwa na lini kampeni zitafanyika na lini wadau watatoa elimu, naomba
tuwe na subira. Tukizingatia sheria hii hakuna ugomvi,”alisema Rais
Kikwete.
Alisema ni vyema kusubiri hadi tume itakapotoa
maelekezo ya utekelezaji huo kwa kuwa muda wa kampeni na utoaji elimu
kwa umma bado.
Rais Kikwete alisema sheria ipo na imepangwa siku maalumu za kufanya hivyo.
Maoni
Chapisha Maoni