Mabilioni escrow mali ya umma

Dodoma.
 Ripoti ya sakata la uchotaji wa Dola za Marekani 200 milioni katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyotua bungeni wiki iliyopita, imeibua mambo mazito baada ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kugundua kuwa fedha zilizochotwa kwenye akaunti hiyo zilikuwa mali ya Tanesco.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh306 bilioni wakati madai ya Tanesco kwa IPTL ni Sh321 bilioni, hivyo fedha zote za Escrow zilipaswa kwenda Tanesco na bado ingekuwa inadai.
Ukaguzi wa akaunti hiyo uliamuliwa na Serikali baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila kudai kuna ufisadi katika uchotaji wa fedha hizo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akaunti hiyo ilifunguliwa baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL.
Katika mgogoro huo, Tanesco ilikuwa inabishia kiwango cha fedha ilichokuwa inalipa kwa gharama za uwekezaji kwa IPTL, ndipo ikaamuliwa na mahakama ifunguliwe akaunti hiyo ili fedha ilizokuwa inalipa ziendelee kuwekwa huko hadi mgogoro utakapokwisha.
Kesi hiyo iliamuliwa katika mazingira yanayoelezwa kuwa na utata na fedha hizo kuchukuliwa haraka na IPTL.
Baada ya ripoti ya uchunguzi huo kukabidhiwa bungeni wiki iliyopita chanzo chetu kimeeleza kuwa kwa mujibu wa ripoti hiyo fedha ni za umma na zilipaswa kwenda Tanesco na shirika hilo kuendelea kuidai IPTL Sh15 bilioni.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Kampuni ya PAP haikununua kihalali asilimia 70 ya hisa za Kampuni ya Mechmar katika IPTL kwani zilizuiliwa na mahakama, hivyo hawana hati halisi ya hisa na kwamba ilifanya udanganyifu katika malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za uongo kuwa walinunua hisa kwa Sh6 milioni badala ya Dola za Marekani 20 milioni, hivyo kuikosesha Serikali Sh8.7 bilioni.
Pia imeeleza kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alivunja sheria kwa kuelekeza kuwa kodi ya ongezeko la thamani kwenye gharama za uwekezaji isilipwe na hivyo kusababisha Serikali kupoteza mapato ya Sh21 bilioni.
“Wizara ya Nishati na Madini haikufanya uchunguzi wa awali (due diligence) kuhusu uhalali wa umiliki wa Kampuni ya IPTL na ilisaini kutoa fedha bila ya kuhakikisha fedha za Tanesco zinarudi na hivyo kusababisha kulipotezea Shirika zaidi ya Sh321 bilioni,” chanzo chetu kilieleza.
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai alipoulizwa juzi baada ya kutoka kwenye Kamati ya Uongozi, bila kufafanua alisema ripoti itawasilishwa bungeni Novemba 26, mwaka huu kama ilivyopangwa na kuwa angetoa taarifa ya kilichojiri kwenye Kamati ya Uongozi bungeni leo.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi wameeleza kuwa, wamekubaliana ripoti hiyo iwasilishwe kama ilivyopangwa na kwamba muda huu ofisi ya Katibu wa Bunge na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) waipitie kwa ajili ya uwasilishwaji.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao