Nyalandu: Hatuna mpango kufukuza Wamasai Loliondo

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema habari zinazodai serikali inataka kuwaondoa wakazi wa zaidi ya 40,000 eneo la Loliondo mkoani Arusha ni za uongo na uchokozi.
Novemba mwaka huu, gazeti The Guardian la nchini Uingereza, liliandika habari kuwa serikali ina mpango wa kuwafukuza Wamasai wanaoishi eneo hilo.
Gazeti hilo lilidai kuwa, lengo ni kuwapatia eneo lenye kilometa za mraba 1,500, kampuni ya OBC ya Falme za Kiarabu.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni jana, Nyalandu alisema habari hizo hazina ukweli wowote.
“Yaani kwamba sisi tunataka tutume maaskari kuwatoa watu kwenye maboma yao tuyachome moto tuwafukuze? Habari hizo ni za uongo, habari hizo zinataka kuipaka tope nchi yetu na ni za uchochezi na mimi nina uhakika wengi wa mashabiki wa habari hizo ni majirani zetu wa nchi jirani,” alisema.
Aliwataka wakazi wa eneo hilo kuishi bila hofu, kwa sababu serikali haina mpango wa kuwaondoa kwenye makazi yao.
“Nami niwahakikishie wanajamii wa Loliondo, Ngorongoro na wanajamii wote wa kimasai ambao wametishiwa nyau, kuwa serikali ya Tanzania haina mpango wowote wa kumfuata kumfukuza mtu yoyote,” alisema.
Alisema mara baada ya Bunge, amepanga kutembelea vijiji hivyo kuzungumza mipango bora ya matumizi ya ardhi, njia bora za kutunza mifugo wakati wa ukame na jinsi ya kuchimba mabwawa.
Nyalandu, alisema lengo jingine la ziara hiyo ni kuzungumza jinsi ya kuhakikisha afya zao na mifugo yao zinakuwa salama.


Aliwapongeza wafugaji wa eneo hilo kwa kuwa sehemu ya uhifadhi na kwamba, Tanzania ni nchi pekee ambayo wafugaji wanaishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na mifugo yao.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji