Matibabu ya Kikwete yazua balaa Bungeni

MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM), kwa mara nyingine tena, jana alinusurika kichapo kutoka kwa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), baada ya kuwapasha kwamba wanatibiwa nchini India, kwanini wanahoji Rais Jakaya Kikwete kutibiwa Marekani.
Kessy alizua kizaazaa hicho wakati Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alipokuwa akijibu miongozo mbalimbali ya wabunge, ukiwemo wa Kessy.
Mbunge huyo ambaye sasa ni mara ya tatu kukwaruzana na wabunge wa CUF kutoka Zanzibar, aliomba mwongozo wa Spika na alipopata nafasi alihoji sababu ya wabunge wa Zanzibar kuhoji matibabu ya Rais Kikwete aliyefanyiwa upasuaji nchini Marekani wakati wao wamekuwa wakitibiwa India kwa gharama za Serikali.
“Mheshimiwa Spika, hawa Wazanzibar wanaohoji Rais Kikwete kutibiwa India, wanakosea sana, mbona wao wanatibiwa India, hatusemi kitu. Nawajua wabunge zaidi ya sita waolitibiwa India, kuna kosa gani Rais Kikwete kutibiwa Marekani, au mlitaka akatibiwe Zanzibar, kwendeni zenu huko,” alimalizia kwa kusema Kessy na hivyo kuibua kizaazaa.
Kauli hiyo ya Kessy iliwaibua wabunge wote wa kambi ya upinzani ambapo baadhi yao walipaza sauti kutaka atolewe bungeni, lakini wabunge wengine wa CUF, wakiongozwa na Khatibu Said Haji (Kondo), walinyanyuka kwenye viti vyao na kumfuata kwenye kiti chake.
Lakini kabla ya kufikiwa, Kessy alisimama na kuchomoka kwa kasi kutoka nje, huku askari wa Bunge wakiwazuia wabunge wa CUF waliokuwa na jazba wasimfuate.
Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM), alifanya kazi kubwa kumzuia mbunge wa Kondo, Khatib ambaye alionekana dhahiri kupania kumtandika Kessy.
Kabla ya Kessy kuanzisha sarakasi hiyo, mbunge wa Viti Maalum, Rukia Kassim Ahamed (CUF), aliomba mwongozo wa Spika kutaka Bunge lisitishe kujadili Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Taifa mwaka wa fedha 2015/2016 ili lipate nafasi ya kujadili deni la Serikali la zaidi ya sh bilioni 100, linalodaiwa na Bohari ya Madawa nchini (MSD), na kusababisha uhaba mkubwa wa dawa kwa wananchi nchini.
Mbunge huyo alisema hakuna sababu ya wao kuendelea kukaa bungeni na kupigwa kiyoyozi huku Rais Kikwete akienda kutibiwa Marekani wakati wananchi vijijini wakipoteza maisha kwa kukosa dawa, kauli ambayo ilimuibua Kessy na kujibu mapigo.
Hii ni mara ya tatu kwa Kessy kutibuana na wabunge wa Zanzibar na kuzua kizaazaa. Mara ya mwisho ilikuwa katika Bunge Maalum la Katiba ambapo mbunge huyo alisema Zanzibar inabebwa katika masuala la Muungano na kwamba haichangii chochote.
Kauli kama hiyo alishawahi kuitoa katika Bunge la Bajeti ambapo alisema Zanzibar inainyonya Tanganyika na kwani haichangii chochote katika masuala ya Muungano, kauli ambayo mara zote imekuwa ikimletea matatizo na wabunge kutoka Zanzibar ambao wanadai ni ya kibaguzi.
Rais Kikwete, amefanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostate), katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu kwa vyombo vya habari juzi ilisema Rais Kikwete amefanyiwa upasuaji huo juzi alfajiri baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake kujiridhisha kuwa alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo.
Inaelezwa kuwa upasuaji huo ulichukua kiasi cha saa moja unusu, umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa na wananchi wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais kwa kadri zitakavyokuwa zinapatikana.
Afya ya JK yaimarika
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana, hali ya Rais Kikwete inaendelea kuimarika na kuwa nzuri huku akiwa ameanza kufanya mazoezi ya kutembea tangu juzi.
“Rais Kikwete ameanza kufanya mazoezi ya kutembea siku ya pili tu baada ya kufanyiwa operesheni. Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, itaendelea kuwapatia wananchi habari sahihi kuhusu maendeleo ya afya yake kadri habari hizo zitakavyokuwa zinapatikana,” ilisema taarifa hiyo.
Rais J Kikwete
Pia, Ikulu iliwashukuru wote ambao wamekuwa wakimwombea Rais Kikwete ili apone haraka na kurejea nyumbani kujiunga na wananchi wenzake katika ujenzi wa taifa.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji