Watanzania waaswa kuchangia elimu
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama, amesema watanzania wanapaswa kuondokana na dhana kuwa jukumu la kutoa elimu bora linapaswa kubebwa na serikali peke yake.
Amesema dhana hiyo ndiyo huwaathiri kwa kiasi kikubwa watoto wa kike na kusababisha kushuka kwa kiwango chao cha elimu, baada ya kuhadaiwa na wanaume wakati wakitoka eneo moja kwenda jingine kwa ajili ya kutafuta elimu.
Mhagama, alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, wakati akiwatunuku vyeti vya utambuzi wadau mbalimbali waliochangia ujenzi wa mabweni kwa ajili ya watoto wa kike kupitia uhamasishaji uliofanywa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
Alisema wananchi wamekuwa hodari kuchangia sherehe zinazotumia gharama kubwa huku wakishindwa kuhimizana kuchangia walau sh 200,000 katika kila kamati kwa ajili ya kuboresha mazingira ya elimu.
“Wanaotunukiwa vyeti leo wamejijengea heshima kubwa katika sekta ya elimu kwa kuwa tupo zaidi ya milioni 40, lakini ni wachache waliojitokeza na hawa kwa nafasi yao wamefanikiwa kuwaepusha mabinti zenu na wale vijogoo ‘fresh’ wanaowaharibia masomo,” alisema Mhagama na kuongeza;
Tuchukulie mfano hapa Dar, kuanzia Alhamisi mpaka Jumamosi ni sherehe na kuna kumbi zaidi ya 200 hivi, kwanini wahusika wasichange walau sh 200,000 kwa ajili ya kumbukumbu yao ya kuinua elimu nchini.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Rosemary Lulabuka, alisema tangu kuanzishwa kwa mfuko wa elimu hadi kufikia Juni mwaka huu, wachangiaji wamefanikiwa kuchanga jumla ya sh bilioni 12.6.
Alisema mahitaji ya elimu nchini ni makubwa kuliko mchango wa serikali na kwamba, kama wadau watajiweka pembeni kutakuwa na tatizo zaidi.
Aliongeza kuwa, kwa kiasi kikubwa waandishi wa habari wamesaidia kutangaza na kuandika matatizo yanayowakabili watoto wa kike, hali iliyoongeza hamasa ya uchangiaji kutoka kwa wadau.
Baadhi ya wachangiaji ni pamoja na benki ya CRDB, Shirika la Nyumba la Taifa, NHC, PPF, PSPF, MMI Steel Mils na wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya, ambao wote walipewa vyeti vitakavyowasaidia kusamehewa sehemu ya kodi katika baadhi ya vitu watakavyoingiza nchini.
Maoni
Chapisha Maoni