‘Acheni kuwabembeleza wawekezaji wasiozingatia sheria za mazingira’
MAOFISA Mazingira katika Wilaya za mikoa ya Iringa na Mbeya wametakiwa kuacha kuwabembeleza wawekezaji wasiozingatia sheria za uhifadhi wa mazingira.
Kauli hiyo, imetolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Constantine Mushi, wakati akifungua mafunzo ya siku tano yaliyoshirikisha maofisa mazingira kutoka Wilaya 14 za mikoa hiyo, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mushi, alisema kuwa wapo baadhi ya wawekezaji katika sekta za madini na nishati wasiozingatia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 inayotaka shughuli yoyote ya maendeleo kuendana na uhifadhi wa mazingira na hivyo kuchangia uharibifu mkubwa wa mazingira.
Alisema kuwa, maofisa mazingira wanatakiwa kusimamia sheria za mazingira kwa kuhakikisha kuwa zinafuatwa, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali wawekezaji wasiozingatia sheria hizo.
Alisema kuwa katika sekta ya nishati, kuna shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi unaoendelea sehemu mbalimbali nchini katika nchi kavu, kwenye ukanda wa bahari, katika maji ya kina kirefu baharini (deep sea), na kwenye maziwa na kusisitiza kuwa, hii ni changamoto kwa maofisa mazingira katika kutoa ushauri na kuhakikisha kuwa binadamu na viumbe wengine hai hawaathiriwi na uwekezaji huo.
Aliongeza kuwa uwekezaji katika sekta ya nishati ni mkubwa, kwani nishati ya umeme ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo suala la mazingira linatakiwa lizingatiwe ili kuhakikisha kuwa wananchi na viumbe wengine hawaathiriwi na uwekezaji huo.
“Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa shughuli zote za maendeleo, zinafanyika bila kuleta athari kubwa katika mazingira yetu kwa kusimamia sheria na kanuni za mazingira pasipokuwa na upendeleo,” alisisitiza Mushi.
Wakati huo huo, Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Gideon Kasege, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwashirikisha maofisa mazingira mpango kazi wa mazingira wa sekta za nishati na madini wa Wizara, kuwapa elimu ya mazingira na kupata michango yao ili kuwa na mkakati wa pamoja wa kuhakikisha sheria na kanuni za mazingira zinafuatwa.
Mhandisi Kasege, alisema kuwa awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ilishirikisha mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Morogoro na Kilimanjaro, awamu ya pili Mwanza, Simiyu, Geita, Mara, Kigoma na Tabora na awamu ya tatu mikoa ya Iringa na Mbeya.
Maoni
Chapisha Maoni