Lipumba aoishauri serikali kuhusu IPTL, deni MSD

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeitaka serikali kuacha mzaha wa kuchezea maisha ya watanzania katika upatikanaji wa mahitaji muhimu, ikiwa ni pamoja na dawa za tiba mbalimbali.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahimu Lipumba, alisema hali ya upatikanaji wa dawa katika zahanati na hospitali inazidi kuwa mbaya kutokana na kushindwa kununua dawa kutoka Bohari ya Dawa (MSD), kutokana na malimbikizo ya madeni.
Alisema hadi kufikia Septemba 2014, MSD inadai hospitali na vituo vya serikali sh bilioni 102 , ambako mwishoni mwa mwaka 2013, deni hilo lilikuwa sh bilioni 76.4.
Alisema sera ya serikali ni vituo vya afya vya serikali kuwapa matibabu bure kina mama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee, watu wenye magonjwa sugu, wasiojiweza pamoja na wenye ulemavu, lakini inashindwa kufanya hivyo.
“Inasikitisha na inaonesha namna gani serikali ya CCM isivyomjali mwananchi wa kawaida, waziri wa afya anapozitaka hospitali kulipa madeni ya bohari ya dawa kwa kutumia nusu ya fedha za uchangiaji zinazolipwa na wananchi, hii ni sawa na kuzieleza hospitali hizo zisitoe huduma bila malipo,” alisema Prof. Lipumba.
Ufisadi wa IPTL
Prof. Lipumba, alizungumzia sakata la IPTL kwa kulihusisha na uchaguzi mkuu, ambako alisema CCM imewawekea fursa wapambe wake kujichotea fedha za umma kupitia fedha zilizowekwa katika akaunti maalum ya Escrow, Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Prof. Lipumba, alisema kama viongozi wa serikali wangekuwa na nia ya dhati ya kuwatumikia watanzania kwa uadilifu, mwaka 2014 mitambo ya IPTL ilitakiwa kuwa ya Tanesco, kwa kuwa mkataba wake na serikali ulikuwa wa miaka 20 ambao unakamilika sasa.
Alisema kuna viongozi wa serikali wanashiriki kuihujumu Tanesco, jambo linaloonyesha jinsi CCM kilivyo chama cha mafisadi kisichokuwa na hata chembe ndogo ya uzalendo.
Alisema CUF inaisubiri  kwa hamu taarifa ya ukaguzi ya mkaguzi mkuu wa serikali wa ‘Tegeta Escrow Account’ na ni matumaini yao CAG ameifanya kazi hiyo kwa uadilifu na weledi wa juu bila woga.
Changamoto kwa serikali ya UKAWA
Prof. Lipumba, alisema serikali ijayo ambayo anaamini itakuwa ya changamoto kubwa, kwani itarithi malimbikizo makubwa ya madeni ya nje na ndani, matumizi mabaya ya fedha za umma na ukosefu mkubwa wa uadilifu na uwajibikaji.


Alisema kwa miaka 10 ijayo, Tanzania inaweza kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 10 na kuongeza ajira kwa vijana na kwamba yote yatawezekana ikiwa kutakuwa na uzalendo wa dhati na kuweka mbele maslahi ya wananchi wa kawaida na kutumia rasilimali na maliasili ya nchi.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao