Tunafundishwa kuchukua sheria mkononi
Mimi nachukia tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Napenda watu tuwe watiifu kwa sheria na linapotokea tatizo, basi taratibu za kisheria zifuatwe. Naamini kwamba huo ndiyo ustaarabu, pia ni njia sahihi ya kuhakikisha kwamba haki inatendeka.
Si unajua, mtu anaweza akapigiwa kelele na mtu mwingine kuwa ‘mwizi’, watu wakatoka na mapanga na mashoka kumrudi mwizi huyo na baada ya kitendo wanang’amua kwamba wala siyo mwizi ila ni mtu wanayemfahamu kwamba ni mlevi na siku hiyo kapotea njia.
Mpaka waling’amue hilo, tayari mtu amekwishaathirika. Yapo mengi ya aina hiyo na sote tunakubaliana kwamba kinachowapata watu hao wasio na hatia siyo kizuri hata kidogo. Waathirika wangepelekwa kwenye vyombo vya sheria, hakika wasingepata madhara waliyoyapata kwa sababu huko ingejulikana huyu alilewa na huyu alipotea, lakini siyo wezi.
Lakini nazungumza hivi kama wasimamizi wa sheria wangefanya kazi zao. Mara nyingi tumeshuhudia namna wanavyoshindwa kuwajibika kwa kutowasikiliza wananchi pale wanaporipoti ukiukwaji wa sheria unaofanywa na wasiopenda ustaarabu.
Wasimamizi hawa wa sheria wanafanya zoezi la kufuata sheria liwe kama ujinga fulani kwani hupati unachokihitaji. Hili ndilo linalowafanya watu sasa watafute njia nyingine ya kujihami na hao wanaovunja sheria na taratibu nayo ni kujichukulia sheria mkononi.
Napata kigugumizi kuwalaumu wananchi wanaojichukulia sheria mkononi baada ya kushindwa kupata majibu kutoka kwa watawala. Hivi karibuni, wananchi wa kijiji kimoja huko Kaskazini, waling’oa mazao ya watu wanaosadikika kuyaotesha kwenye vyanzo vya maji. Kwa kuotesha mazao katika maeneo hayo, maji yalipungua na watu wakaathirika.
Sasa, sijui kama ingekuwa ni busara wao kusubiri mpaka vyanzo hivyo vikauke kabisa halafu ndiyo wakae kwenye vikao wakilalamikia watu waliootesha mazao yao huko? Siyo vyema kutamka, lakini mimi nafikiri utawala ulioziba masikio kuhusu jambo hilo, ndiyo uliotoa ruhusa kwa wananchi hao kujichukulia sheria mkononi.
Tena walichonifurahisha ni kwamba, baada ya kung’oa wakapanda miti, kisha kuweka ulinzi kuhakikisha kwamba wapuuzi hao wanaolima kwenye vyanzo vya maji hawarudi tena. Hii ni aibu kwa watawala husika. Yaani watawala wa eneo husika wanapozidiwa nguvu na wapuuzi wakati wana mamlaka na sheria inayowapa nguvu kuchukua hatua, halafu wananchi wanawaweza wapuuzi hao, tujiuize kuna utawala kweli hapo?
Picha inajichora vizuri ni kwamba, watu wanajiongoza wenyewe. Tena cha kushangaza, hakuna mtawala aliyefungua kinywa chake kana kwamba wanaiambia jamii “nyie endeleeni tu” Nadhani na sisi wa mjini tunapatiwa funzo hapa kwamba kwa yale yanayotukera, ambayo watawala wa eneo husika wameshindwa kuchukua hatua na tunaamini tutaathirika, basi tuchukue hatua wenyewe. Mimi naijua shule jirani yangu ambayo uongozi wake umeamua kupunguza gharama za kuhudumia maji taka kwa kuyatiririsha kwenye jamii, badala ya kunyonya kwa magari na kuyapeleka huko yanakotakiwa kumwagwa.
Jamii imeshaonana na uongozi wa shule, wameshapeleka malalamiko yao Serikali ya Mtaa, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa na wakuu hao wanasubiri kukiwa kumetulia kidogo basi watatiririsha tena.
Hivi tukinyanyuka siku moja kwa mapanga na virungu tukaenda kuvunjavunja majengo na vifaa vya shule hiyo tutaambiwa tumechukua sheria mkononi?
Najua tutaambiwa Serikali ya mtaa iliposhindwa, basi tungepeleka kata, kutoka kata, twenda wilaya na kadhalika mpaka sijui tufike kwa Rais ndipo ionekane kwamba hapo tumefuata sheria? Kwa nini usumbufu wote huo?
Maoni
Chapisha Maoni