Watoto 60 wachunguzwa moyo Muhimbili
JUMLA ya watoto 60 wamefanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo bure, Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na watakaobainika watapatiwa matibabu.
Watoto hao ni wale ambao wazazi wao wanakipato cha chini, ambapo mdhamini mkubwa wa matibabu hayo ni Shirika la Kimataifa Compassio Tanzania wakishirikiana na Kanisa la Methodist.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es salaam jana, Askofu wa Kanisa la Methodist, Methodius Yamugu, alisema kwa kutambua umuhimu wa watoto, wameamua kuanzisha makambi ya uchunguzi wa afya ya moyo kwa vijana na watoto.
Yamugu alisema wameamua kuanzisha uchunguzi huo kutokana na ukweli kwamba maradhi hayo yanaonekana kuwa changamoto kubwa hususan katika baadhi ya familia duni.
“Utaratibu wa kuwapata watoto hawa unaanzia katika serikali za mitaa lengo likiwa ni kuwapata watoto ambao kweli wanavigezo vinavyohitajika na kwamba hakuna ubaguzi wa dini.
Naye kiongozi wa timu ya madaktari hao, Dk. Tatizo Wanne, alisema matatizo ya moyo yako ya aina mbili, akibainisha kuwa kuna ya kuzaliwa nayo ama yale anayopata mtoto baada ya kuzaliwa.
Alisema ili kuzuia mtoto asiweze kuzaliwa na matatizo hayo ni vema wazazi wakawa makini katika kufuatilia huduma za chanjo zinazotolewa kwa ajili ya kuzui maradhi hayo, mfano mzuri ni ile surua lubela iliyotolewa hivi karibuni.
Alitoa wito kwa Watanzani kuwa ni lazima wakajijengea utaratibu wa kufika kwenye vituo vya afya kwa lengo la kuchunguza afya zao pindi watakapobainika kuwa na maradhi wapatiwe matibabu haraka.
Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la Compassion, Elieshi Kisinza, alisema ili nchi iweze kuwa na usalama katika maeneo yote, ni vema watanzania wawekeza nguvu zao kwenye watoto.
Maoni
Chapisha Maoni