Tacaids: Maadhimisho ya Ukimwi kuhakikisha azma ya sifuri tatu inafikiwa
TUME ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), imesema kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani mwaka huu imelenga kutoa msukumo wa utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti Ukimwi.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti Mtendaji wa Tacaids, Dk. Fatma Mrisho, alisema kauli mbiu hiyo pia inalenga kudhibiti Ukimwi Kitaifa na Kimataifa ili kufikia azma ya sifuri tatu.
Dk. Fatma alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni Tanzania bila maambukizi mapya ya VVU, vifo vitokanavyo na Ukimwi, ubaguzi na unyanyapaa inawezekana.
Alisema kauli mbiu hiyo inahimiza utekelezaji wa dahati wa malengo ya maendeleo ya millennia na maazimio yaliyowekwa kwenye mkutano maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukimwi.
“Azma ya sifuri tatu ni kuhakikisha maambukizi mapya ni sifuri,vifo vitokanavyo na Ukimwi sifuri na unyanyapaa sifuri ifikapo mwaka 2018,”alisema.
Pia alisema maadhimisho ya mwaka huu kitaifa yatafanyika mkoani Njombe kuanzia Novemba 24 na kufikia kilele Desemba mosi, mwaka huu.
Akizitaja shughuli zitakazofanyika ni pamoja na maonyesho ya shughuli za wadau wa udhibiti wa Ukimwi, kongamano la kitaifa la kutathimini hali na mwelekeo wa ukimwi, upimaji wa hiariwa VVU na ushauri nasaha.
Alisema maadhimisho hayo yatatoa tathimini ya hali halisi na mwelekeo wa udhibiti wa Ukimwi na kubaini changamoto, mafanikio na mikakati katika kupambana na janga hilo.
Aidha aliwataka wananchi kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya nchi ambapo maadhimisho hayo yatafanyika na kupata elimu mbalimbali ikiwemo inayohusu kujinga na maambukizi ya Ukimwi.
Maoni
Chapisha Maoni