mwanzo Ajali yaua 12 Morogoro
Morogoro. Watu 12 wamefariki dunia papohapo na
wengine ambao idadi yao haijafahamika wamejeruhiwa baada ya basi
walilokuwa wakisafiria kugonga treni ya abiria eneo la Kiberege,
Ifakara Wilaya ya Kilombero.
Ajali hiyo iliyohusisha basi la Kampuni ya Aljabir ilitokea jana saa 9:15 alasiri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo
alisema miongoni mwa waliokufa katika ajali hiyo, sita ni wanaume, wanne
wanawake na watoto wawili mmoja wa kike na mwingine wa kiume. Paulo
aliwataja marehemu watatu waliotambulika kuwa ni Frugensia Lusangila
(60) na Albeta Lusangila (62) wakazi wa Ichonde Tarafa ya Mang’ula na
Joseph Kazwila (34) mkazi wa Dar es Salaam.
Akielezea chanzo cha ajali hiyo Kamanda Paulo
alisema, dereva wa basi hilo alivuka barabara yenye makutano na reli
bila ya kuchukua tahadhari na kuigonga treni.
Alisema kuwa majeruhi wa ajali hiyo wamepelekwa
katika Hospitali ya Mtakatifu Francis Ifakara na Kituo cha Afya Kibaoni
kwa matibabu.
Alisema dereva wa basi hilo alikimbia mara baada ya ajali hiyo kutokea na polisi wanaendelea kumtafuta.
Maoni
Chapisha Maoni