Ulinzi miundombinu ya DART waungwa mkono
Pendekezo la Kamati ya kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (Tamisemi) kuharakisha uundwaji wa Kikosi Kazi cha ulinzi kwenye miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka limeungwa mkono.
Hivi karibuni, kamati hiyo katika kikao chake na Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ilitoa pendekezo kwa uongozi wa wakala huo kuzungumza na jeshi la polisi kuona jinsi ya kuunda kikosi kitakachohusika na ulinzi wa miundombinu hiyo inayoharibiwa.
Wajumbe wanaounda kikundi kazi cha mawasiliano na utoaji elimu kwa umma katika kikao chao cha hivi karibuni kwa pamoja wameunga mkono agizo la kamati ya Tamisemi na kuahidi kuendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo ya DART.
Kikundi kazi hicho kinaundwa na maofisa habari kutoka taasisi mbalimbali ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na mradi huo. Pia Askari wa Usalama Barabarani wanakuwa na uwakilishi kwenye vikao vya maofisa habari na mawasiliano wa mradi.
“Naamini mjumuiko huu utasaidia katika kuleta uhamasishaji mkubwa katika maeneo yetu, maana tatizo hili limekuwa kubwa na linaendelea kushika kasi,” alisema Mkurugenzi wa Utawala, Rasilimali Watu na Mawasiliano wa DART, Evodius Katare.
Katare alisema anaamini uwepo wa vyombo vya usalama katika kikosi kazi hicho kutarahisisha suala la kulinda miundombinu hiyo hasa kwa kushirikiana na viongozi walioko katika ngazi za mtaa, kata na hata wilaya, ili kukomesha hujuma zinazoendelea.
Alisema hatua inayofuata ni kuandaa kikao cha pamoja kati ya Wakala, maafisa habari wanaohusika katika mradi na jeshi la polisi ili kutafuta njia nzuri ya kuweza kukabiliana na watu wanaohujumu na wale wanaofanya biashara katika eneo hilo kinyume na sheria.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya kipolisi ya Magomeni (OCD), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Anyimile Nsemwa alisema kwa ushirika huo kazi ya kuwaondoa watu katika maeneo hayo itakuwa rahisi kwao.
Mbali na kuunga mkono kamati ya bunge, Mkuu wa Mawasiliano wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bw.Gaston Makwembe alisema atafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa mradi na faida zake.
Maoni
Chapisha Maoni