Serikali kuimarisha huduma za kifedha
SERIKALI imedhamiria kuimarisha upatikanaji wa huduma za fedha nchini, ili kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2016.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alisema hayo mjini Dodoma Juzi wakati wa uzinduzi wa huduma ya ‘Airtel Money Timiza’ yenye lengo la kuwapatia mikopo wateja kwa kupitia simu zao za mkononi.
Alisema huduma ya ‘Airtel Money Timiza inayoshirikiana na kampuni ya Pan-African (AFB) ni mpya Afrika na duniani kote ambapo itawasaidia wateja kupata mikopo ya muda mfupi.
Profesa Mbarawa alisema takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha hadi sasa kuna taasisi 52 zinazojihusiaha na utoaji wa huduma za kifedha, hivyo kuchangia upatikanaji mdogo wa huduma za kifedha.
“…Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2013 na 2014 kulikuwa watumiaji wa simu wapatao 972,600,000 ambao hukamilisha miamala mbalimbali kwa kutumia simu za mikononi kufanya manunuzi yanayofikia trilioni 28.3,” alisema.
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa aliisifu kampuni ya Airtel kwa uvumbuzi wao ambao pia utachangia kasi ya ukuaji wa uchumi kwa njia ya mawasiliano.
Akizungumzia huduma ya ‘Airtel Money Timiza’, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Sunil Colaso alisema ili kupata huduma hiyo mteja hatatakiwa kuweka amana yeyote ile, lakini pia mhusika atatakiwa kulipa mkopo wake kwa wakati na kuseama kuwa kuna mkopo wa siku 7,14 na 28.
Maoni
Chapisha Maoni