Mauaji tena Kiteto, Serikali yawaangukia viongozi wa siasa

WAKATI mkulima Hassan Kondeya ameuawa jana na kundi la wafugaji wa kabila la Masai, Serikali imetoa kauli kuhusiana na hali tete ya mauaji ya mara kwa mara wilayani humo.

Akitoa tamko maalum la Serikali jana Bungeni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema kuwa Serikali inawataka viongozi wa siasa kuchukua hatua kuhakikisha suluhu ya kudumu inapatikana Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.

Alisema jeshi la polisi linaendelea kudhibiti hali ya usalama katika Kijiji cha Matui wilayani humo ambako juzi mapigano hayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya wanne na wengine kujeruhiwa.

“Hali bado ni tete wilayani Kiteto ni wajibu wa viongozi wa siasa kuchukua hatua kuhakikisha suluhu ya kudumu inapatikana Kiteto,” alisema Chikawe.
Akizungumzia mauaji katika Kijiji cha Matui, alisema mwanakijiji Mzee Kodenya alikwenda kulalamika kituo cha Polisi kwamba, kuna wafugaji jamii ya Kimasai wameingiza ng’ombe katika shamba lake la mihogo.
“Alifika katika kituo cha polisi jioni na kuwaeleza, lakini baadaye alisema kwa kuwa anawafahamu wahusika, ataenda kuzungumza nao ili wayamalize. Aliamua hivyo kutokana na mkutano wa wakulima na wafugaji ambao walikubaliana kwamba kukiwa na jambo lolote ni vyema wakae na kutatua, hivyo polisi walikubali aende kufanya hivyo,” alisema Waziri Chikawe.

Alisema juzi Mzee huyo alikutwa amefariki dunia, mwili wake ukiwa umefukiwa kiwiliwili huku kichwa kikiwa nje katika shamba lake hilo la mihogo.

Chikawe, alisema kutoka na mauaji hayo, kabila la ndugu wa marehemu Kondenya, walikusanyika na kuvamia maboma ya wafugaji.
“Walivamia kubomoa maboma ya wafugaji, wakachoma moto na kuswaga mifugo na kuondoka nayo, huku wakiwatuhumu wamasai kuhusika na mauaji ya ndugu yao…

Wakati wakiendelea na uhalifu huo, walikutana na mama mmoja wa kimasai akiwa amebeba mtoto wake wa kiume wa miaka minne, walimkatakata mama huyo kwa mapanga na kumuua huku wakimuacha mtoto akiwa salama,” alisema Chikawe.
Aidha, alisema kutokana na mauaji hayo, wafugaji walianzisha mapigano na kusababisha vifo vya watu wanne.
Hata hivyo, alisema uongozi wa Mkoa wa Manyara pamoja na wa Wilaya ya Kiteto, walifika katika kijiji hicho na bado wapo hadi sasa, wakijitahidi kurudisha hali ya amani na kufanya uchunguzi kubaini waliohusika na uhalifu huo ili waweze kuchukuliwa hatua.

Aidha, alisema Jeshi la polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano katika eneo la kijiji cha Chitego Wilaya ya Kongwa wakiwa na ng’ombe 121 walioibiwa na kufikisha jumla ya ng’ombe 309 waliokamatwa.
Kauli ya Serikali, imekuja siku mbili baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kulieleza Bunge kuwa hali ya maisha Kiteto inatisha kutokana na mauaji ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji.


Alisema ukifika Kiteto, huwezi kuamini kama ni sehemu ya Tanzania, kwani watu wanamiliki silaha watakavyo kana kwamba hakuna Serikali.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji