Ziara ya Rais wa China kizaazaa Dar
Rais wa china Xi Jinping |
Ripoti iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya Uingereza inayojihusisha na uchunguzi wa masuala ya mazingira, inadai kuwa maofisa hao walinunua kiasi kikubwa cha bidhaa hizo katika soko la Mwenge, Dar es Salaam, kisha kuzisafirisha kidiplomasia kwa ndege ya rais huyo.
Taasisi hiyo iitwayo Environmental Investigation Agency (Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira– EIA), katika ripoti hiyo inasema maofisa hao walitumia fursa ya kidiplomasia ya kutokukaguliwa kwa mizigo yao, kupitisha bidhaa hizo haramu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).
Biashara ya meno ya tembo ilizuiwa kimataifa tangu
mwaka 1989 kwa kusainiwa kwa azimio la kulinda viumbe walio hatarini
(Cites), azimio ambalo pia limesainiwa na China na Tanzania.
Taarifa hiyo iliandikwa kwa mara ya kwanza jana na Gazeti la New York Times la Marekani na baadaye kuwa moja ya habari zilizopewa uzito wa juu katika vyombo vingine vya habari vya kimataifa, huku Kituo cha Televisheni cha Shirika la Habari la Uingereza BBC, kikijadili kwa kina kashfa hiyo iliyopewa jina la “ndege ya rais kutumika kusafirisha meno ya tembo”.
BBC katika taarifa yake ilitumia picha za meno ya tembo na zile za maktaba ambazo zilikuwa zikimwonyesha Rais Jinping akilakiwa na Rais Jakaya Kikwete pamoja na viongozi wengine wa Tanzania alipowasili nchini kwa ziara hiyo.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema jana kwamba Serikali haifahamu chochote kuhusu tuhuma hizo na kwamba hata kama zingekuwa na ukweli ndani yake waliopaswa kuulizwa ni Serikali ya China.
“Serikali haina evidence (ushahidi) wowote
unaoonyesha kwamba suala la aina hii lilitokea, lakini pili mimi siamini
kama kweli maofisa wa China walifanya kitendo hiki na kama hicho
kilifanyika basi wanaopaswa kuulizwa ni Serikali ya China,” alisema
Balozi Sefue na kuongeza:
“Siamini kama madai hayo ni ya kweli kwa sababu
maofisa wanaosafiri na viongozi hukaguliwa, kwa nini wasikaguliwe na
China ni marafiki zetu wazuri tu? Kwa hiyo sisi kama Serikali hilo jambo
hatulifahamu kabisa.”
Baada ya kutangazwa katika vyombo vya habari vya kimataifa, maofisa wa Serikali ya China wamekanusha tuhuma hizo wakisema, “hazina ukweli wowote” wala ushahidi wa kuzithibitisha.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Hong
Lei alinukuliwa na Shirika la Habari la Associated Press (AP) akisema:
“Ripoti hiyo haina ushahidi wowote na hatukufurahishwa kabisa na taarifa
hizi.”
Maoni
Chapisha Maoni