Dr.Shein – Hakuna mamlaka kamili Zanzibar!

Dr A. Shein Rais wa Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema ndoto za wapinzani kutaka kuvunja Muungano kwa kutumia visingizio vya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili, hazitofanikiwa na kuwataka kusahau mpango huo.
Akizungumza na wananchi wa mikoa miwili katika mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba jana, alisema

Serikali anayoiongoza yeye inafuata makubaliano ya Hati za Muungano ya mwaka 1964.
Katika mkutano huo alioutumia kufafanua mafanikio ya miaka minne ya kuwepo madarakani na Katiba Inayopendekeza, Dk Shein alisema makubaliano hayo yanahusu muundo wa Muungano wa serikali mbili.
“Wapo watu wanadai Zanzibar kuwa na mamlaka kamili…huwezi kuwa na mamlaka kamili kwa mujibu wa Hati ya Muungano ya mwaka 1964…kufanya hivyo ni kuvunja Muungano,” alisema.

Alisema, kwa bahati mbaya, wapinzani wamekuwa wakitumia nafasi ya kupotosha wananchi wa Pemba, hata kwa mambo yenye maslahi ambayo yamelenga kuimarisha uchumi na kukuza maendeleo.
“Mimi nashangaa sana hawa wapinzani, walikimbia katika mchakato wa Katiba na sasa wapo vichochoroni wakifanya kazi ya kupotosha ukweli uliopo,” alisema.

Kwa mfano alisema kwa bahati mbaya, anasikitika kuwa baadhi ya mawaziri wake, wamekuwa wakiongoza kwa upotoshaji wa hali ya juu kwa mambo ambayo wanafahamu ukweli wake.
“Nasikitika sana wananchi… wapo baadhi ya viongozi katika Serikali ninayoiongoza ni vigeugeu wa hali ya juu, sijui kwa nini jamani,” alisema Dk Shein kwa masikitiko.

Akifafanua, alisema wapo waliotaka muundo wa Muungano wa Mkataba, ambao umekataliwa kwa sababu hauna maslahi na unaweza kuvunja Muungano wa serikali mbili.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ipo kwa mujibu wa sheria ikiwa na mihimili yake yote mitatu, ikiwemo Rais, Mahakama na Baraza la kutunga Sheria. “Sasa huyu anayesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina mamlaka nani? Utakuwaje Rais wa Zanzibar kama huna mamlaka ya nchi?” alihoji.

Aliwataka wananchi wa Pemba, kujitokeza kwa wingi kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa wakati ukifika, kwani katiba hiyo ndiyo mkombozi kwa wananchi wa Zanzibar, itakayoimarisha umoja na utulivu na kuleta maendeleo ya wananchi wote.

Dk Shein alisema kisiwa cha Pemba sasa kimebadilika kwa kiwango kikubwa, kutokana na mabadiliko yanayoletwa siku hadisiku, ikiwemo kuimarishwa kwa miundo mbinu na nishati ya umeme.
“CCM ndiyo chama kinachozingatia maendeleo na kuleta mabadiliko ya wananchi wa Unguja na Pemba ambapo hata washiriki wa maendeleo wanatupongeza kila siku,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Hamad Bakari Mshindo, alisema wananchi wa Pemba wapo tayari kupigia kura Katiba Inayopendekezwa wakati ukifika. “Nawaomba Wapemba wenzangu, msikubali kupotoshwa na kudanganywa na wapinzani wanaosema kwamba Katiba Inayopendekezwa haina maslahi kwa wananchi wa Zanziba…si kweli,” alisema.
Alisema Katiba Inayopendekezwa imetoa fursa kubwa kwa wananchi wa Zanzibar na kufaidika katika maeneo mbali mbali ikiwemo ardhi, elimu na mambo ya uchumi.
=======================================================================

Maelfu ya wananchi wa kisiwani Pemba waliohudhuria Mkutano huo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Zanzibar akisalimina na Viongozi mbali mbali alipowasili katika uwanja wa Ndege wa Karume, Pemba.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia Makamu Mwenyekiti wa CCM-Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein(katikati) Naibu katibu Mkuu wa CCM-Zanzibar, Vuai Ali Vuai (wa tatu kushoto) Makamu wa Pili wa Rais na pia Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM

Taifa(NEC), Balozi Seif Ali Iddi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Abdalla mohamed Mshindo na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mama Asha Balozi wakiwa katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika uwanja Gombani ya Kale, Pemba
Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,

Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na maelfu ya wananchi wa Mikoa ya Pemba katika Uwanja wa Gombani ya kale, Kisiwani Pemba
Makamu Mwenyekiti wa CCM-Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la

Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein akionesha Katiba Inayopendekezwa wakati akizungumza na wananchi wa Mikoa ya Pemba katika Uwanja wa Gombani ya Kale, Kisiwani Pemba
Baadhi ya wananchi wa kisiwani Pemba wakisikiliza kwa makini hoja za viongozi mbali mbali katika mkutano uliofanyika katika uwanja gombani ya kale, Wilayani Chake chake, Pemba

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao