‘Tamisemi isisimamie uchaguzi’
Dar es Salaam.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimependekeza Sheria ya Uchaguzi Serikali za Mitaa ibadilishwe ili uchaguzi huo usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) badala ya kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Pia kituo hicho kimetaka watendaji wa Tamisemi waliosababisha uchaguzi huo kuvurugika wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Hata hivyo, habari zilizopatikana jana jioni zilisema, Tamisemi imeshawachukuliwa hatua za kinidhamu baadhi ya watendaji wake waliosababisha kuvurugika kwa uchaguzi huo.
Hatua hiyo ya LHRC imekuja baada ya kufanya uangalizi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika mikoa 25 na kubaini kasoro nyingi.
Naibu Mkurugenzi wa LHRC, Ezekiel Masanja alisema makosa yaliyojitokeza kwenye uchaguzi huo ni kwa sababu ya Tamisemi kutokuwa na uelewa wa masuala ya uchaguzi.
Alisema kitendo cha uchaguzi kuvurugika na kurudiwa ni hasara kubwa iliyosababishwa na watendaji wazembe wa Tamisemi.
Pia, vifaa kutofikishwa kwa wakati kwenye vituo vya kupigia kura na kusababisha uchaguzi huo kuahirishwa ni jambo lingine lisilopaswa kuvumiliwa.
Maoni
Chapisha Maoni