Tumekomaa Sh306 bil za escrow na hizi Sh682 bilioni?
Ilikuwa wiki ya aina yake, wiki ya mipasho na kila mmoja ameshuhudia kile kinacholiliwa katika kukabiliana na ufisadi katika Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo kila mmoja alitamani kuona mwisho wake.
Ni mlolongo mpana hasa baada ya Ripoti ya CAG kubaini ‘shimo’ lililokuwa limejaaa noti lililokuwa kimbilio la kila mmoja anayeweza kulifikia. Hatimaye uamuzi wa nini kifanyike umetolewa.
Sitaki kuingia sana kwenye escrow kwa kuwa timbwili lake linafahamika na kila mmoja anasubiri nini kitafuata baada ya taarifa ya mwisho.
Japokuwa nimechelewa kuisemea, lakini ninaamini bado niko kwenye mstari, hili la vito vya tanzanite. kwamba nchi nyingine zinajivunia ‘ujiko’ wa Tanzania kwa kuongoza duniani kwa madini yetu wakati sisi wenyewe ni hohehahe.
Wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya vito mjini Arusha, naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava na Kamishina wa Madini nchini, Paul Masanja walisema Tanzania inauza asilimia 20 pekee ya madini ya tanzanite na asilimia 80 iliyosalia ikiuzwa na Kenya na India.
Tulielezwa kuwa Kenya iliuza tanzanite yenye thamani ya zaidi ya Sh173 bilioni, India Sh509 bilioni, Tanzania iliuza Sh48.5 bilioni pekee katika soko la dunia. Kwa kweli nilipigwa na butwaa kwa hili. Nilishangaa na pengine wapo wanaonishangaa ninaposhangaa. Lakini sitaacha kusema.
Nilishangazwa na taarifa nyingine ya baadaye kuwa eti Serikali itatumia Polisi wa Kimataifa (Interpol), kukabiliana na utoroshaji madini ya tanzanite nje ya nchi.
Haya sasa yanasemwa na mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Madini, Richard Kasesela ambaye anasema Serikali imefikia hatua hiyo baada ya kuchunguza na kubaini njia na mbinu zote zinazotumika kutorosha madini hayo nje ya nchi.
“Kuanzia sasa, yeyote atakayekutwa akiuza tanzanite nje ya nchi bila cheti cha uhalisia kinachothibitishwa yametoka Tanzania kupitia njia halali, atakamatwa na kurejeshwa nchini na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi”, ni kauli ya Kasesela
Nilijiuliza, hivi siku zote walikuwa wapi hadi leo kukumbuka hayo ya Interpol? Inawezekana pia Interpol wakawa hawajui a, b, c ya kinachoendelea pamoja na kauli za kutia matumaini kutolewa na ikawa siasa tu.
Kwa jinsi ninavyoamini, hawajaambiwa waanzie wapi, na si kwa madini hayo pekee, kuna madini mengi yanatoroshwa. Kuna tani na tani za mchanga wa madini tunaambiwa zinakwenda kupembuliwa huko, sisi tunabaki na mashimo.
Hivi mtu avune mpunga shambani kwako, halafu anakwambia atafanya kazi ya kukoboa kisha akuletee mchele, si utaletewa pumba?
Mujibu wa Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni