Miundombinu Ustawi wa Jamii kuboreshwa

SERIKALI imeahidi kulitafutia ufumbuzi tatizo la miundombinu linaloikabili Taasisi ya Ustawi wa Jamii ili kukabiliana na ongezeko kubwa la wanafunzi kila mwaka katika Taasisi hiyo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika mahafali ya 38 ya  Taasisi  ya Utawi wa Jamii, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashidi, alisema ofisi yake inaangalia uwezekano wa kulimaliza tatizo la miundombinu katika  Taasisi hiyo ya elimu ya juu ili kuendana na ukuaji wake.
Alisema katika utekelezaji wa hilo, Wizara yake itaangalia uwezekano wa kuikabidhi Taasisi baadhi ya majengo ya mikoani yanayomlikiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ili Taasisi iweze kupanua huduma zake hadi mikoani.
“Ofisi yangu italishughulikia suala hili kwa umakini mkubwa ili majengo yaliyo chini ya wizara yangu hasa yale yaliyopo mikoani, na ambayo wizara kwa sasa haiyatumii  mkabidhiwe ili muendelee kupanua huduma za utoaji wa elimu  ikiwa ni hatua ya kukabiliana na ongezeko la udahili,” alisema Rashidi.
Pia, Waziri Seif aliitaka Taasisi hiyo kuendelea kufanya tafiti  katika nyanja mbalimbali hasa katika maeneo ya manejimenti ya rasilimali watu, uongozi kazi na ustawi wa jamii, zitakazoibua changamoto kwa lengo la kuleta ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya magavana wa Taasisi hiyo, Prof. Lucian Msambichaka, alisema Taasisi  mwaka huu  imeanzisha shahada ya uzamili katika fani ya ustawi wa jamii, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).
Naye mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Abu Mvungi, alimwambia mgeni rasmi kuwa, licha ya changamoto zinazoikabili Taasisi  hiyo, bado imeendelea kutekeleza kwa ubora wa hali ya juu majukumu yake makuu matatu ambayo ni mafunzo, utafiti na kutoa ushauri weledi .


Katika mahafali hayo ya 38, wahitimu 1,225 walitunukiwa  tuzo zao katika fani za menejimenti ya rasilimali watu, uongozi kazi na ustawi wa jamii kwa kiwango cha astashahada, stashahada, shahada na stashahada ya uzamili.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao