Wafungwa 887 huru
Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 887 wakati wa kuadhimisha miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema katika taarifa yake jana kuwa Rais kwa kutumia madaraka yake kikatiba, ametoa msamaha huo na kuwapunguzia vifungo wafungwa 4,082 ambao watabaki gerezani wakitumikia muda uliosalia.
Hata hivyo, msamaha huo hautawahusu wenye makosa ya ufisadi na uharibifu wa miundombinu. Pia, hautawahusu waliofungwa kwa kutumia vibaya madaraka yao, biashara haramu ya kusafirisha binadamu, kupatikana na nyara za Serikali, ubadhirifu wa fedha za umma, ugaidi, uharamia na ama kupokea au kutoa rushwa.
Wengine ambao hawatahusika na msamaha huo ni wale waliohukumiwa kunyongwa, kifungo cha maisha, biashara za dawa za kulevya, unyang’anyi wa kutumia silaha, kupatikana na silaha au risasi na kunajisi.
Wengine ni wenye makosa ya kubaka au kulawiti, kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wanaotumikia kifungo chini ya sheria ya bodi ya Parole, sheria ya huduma kwa jamii na waliowahi kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi.
Waliosamehewa na kupunguziwa adhabu
Waziri Chikawe aliwataja walioachiwa huru kuwa ni wafungwa ambao ni wagonjwa wa Ukimwi, kifua kikuu na saratani ambao wako kwenye ‘hatua za mwisho kumaliza vifungo na ambao watathibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya.
Wengine ni wazee wenye miaka 70 au zaidi, wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili na wafungwa wa kike walioingia gerezani na mimba, watoto wanaonyonya na wasionyonya. Baadhi ya wafungwa wamepunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao.
Maoni
Chapisha Maoni