JK akatisha ziara ya Pinda Uarabuni

Dubai. U.A.E
Rais Jakaya Kikwete akiteta jambo na Waziri Mkuu Mizengo Peter Pinda, hivi karibuni. Picha na Maktaba 
. Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekatiza kwa muda, ziara yake katika Falme za Kiarabu kwa maelezo kwamba ameitwa nyumbani na Rais Jakaya Kikwete kwa shughuli maalumu.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika ziara ya kutembelea nchi za Falme za Kiarabu, ikiwa ni sehemu ya kudumisha ushirikiano na kutafuta wawekezaji, amekatisha ziara hiyo siku mbili baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kujiuzulu kutokana na kashfa ya Escrow.
Werema alijiuzulu juzi na Rais Kikwete akaridhia hatua hiyo, huku umma ukisubiri hatua zaidi dhidi ya mawaziri na watendaji wa Serikali waliotajwa katika sakata hilo.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Jaji Werema alisema ushauri wake wa kisheria kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow haukueleweka na hivyo kuchafua hali ya hewa.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, leo Waziri Mkuu alitarajiwa kufanya mazungumzo na washiriki wa maonyesho ya B2B pamoja na kutembelea maeneo mengine lakini ziara hiyo imefutwa na badala yake anaondoka asubuhi kurudi nyumbani.
Baadaye leo Pinda alitakiwa kwenda Doha, Qatar kwa ziara kama hiyo hadi Desemba 23.
Baada ya kukamilisha jukumu aliloitiwa, Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea Falme za Kiarabu Jumamosi kuendelea na ziara yake.
Chadema yakerwa JK kumsifia Werema
Jana, Chadema kilielezea kusikitishwa kwake na sifa alizotoa Rais Kikwete kwa Jaji Werema kuwa ni mwaminifu na mwadilifu wakati amejiuzulu kutokana na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema kitendo cha Rais kumsifu Jaji Werema kinawakatisha tamaa Watanzania.
“Hakupaswa kupongezwa badala yake Rais angemwambia kwamba alikuwa kwenye taratibu za kumfukuza kazi,” alisema Mnyika na kuongeza kuwa hata watuhumiwa wengine katika kashfa hiyo wanaposikia Rais akimpongeza mwenzao wanaona makosa yao ni jambo la kawaida linaloweza kupongezwa.


“Hata vyombo vya dola vitaogopa kumshtaki Werema kwa sababu amepongezwa na Rais kwamba ni mtumishi ambaye alikuwa mwaminifu na mwadilifu,” alisema Mnyika.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao